Tanzania yaahidi Mazingira mazuri ya Uwekezaji Sekta ya Madini
Teresia
Mhagama na Devotha Myombe
Tanzania imeahidi
kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini kama
ilivyoainishwa katika Sera ya Madini ya mwaka 2009.
Hayo yameelezwa na
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe wakati wa
semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na
Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya
Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini
iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji endelevu wa
rasilimali madini nchini.
Alisema kuwa, Dira ya
Maendeleo ya Mwaka 2025 imelenga katika kuanzisha migodi mikubwa, ya kati na
midogo inayoendeshwa kwa kuzingatia usalama na utunzaji wa mazingira hivyo
mazingira mazuri ya uwekezaji yatavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza ili
kuendeleza Sekta ya Madini nchini.
Profesa Mdoe alisema
kuwa semina hiyo ililenga katika kupata taarifa zilizohuishwa kutoka Japan na
Tanzania kuhusu shughuli za utafiti na utunzaji wa mazingira katika Sekta ya Madini
nchini na kujadiliana juu ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi husika.
“Semina hii ni muhimu
kwani Taasisi hizi zitajadiliana kuhusu kuendeleza ushirikiano katika sekta
hii, kufahamu fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya Madini kwani wadau kutoka
Tanzania na Japan wataweza kupata taarifa za utafiti kuhusu madini yaliyopo
nchini na pia Taasisi ya JOGMEC itapata fursa ya kueleza shughuli zake barani
Afrika,” alisema Profesa Mdoe.
Akieleza kuhusu Sekta
ya Madini nchini, Profesa Mdoe alisema kuwa Sekta hiyo kwa sasa inachangia
asilimia 3.5 katika Pato la Taifa na
kueleza kuwa asilimia hiyo bado ni ndogo kwani lengo la Serikali ni kuona kuwa
Sekta hiyo inachangia mpaka asilimia 10 kufikia mwaka 2025.
Hata hivyo Profesa
Mdoe alisema kuwa ili sekta hiyo ichangie ipasavyo katika Uchumi wa Taifa,
kutategemea kutoshuka kwa bei ya bidhaa zinazotokana rasilimali madini na uchumi wa dunia kuendelea kukua ili
makampuni yanayojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa madini yapate fedha
kutoka Taasisi za kifedha duniani ili kuanzisha shughuli za utafiti na
uchimbaji wa madini.
Aidha Profesa Mdoe
aliwaalika wawekezaji kujenga vituo vitakavyotumika katika shughuli za
uongezaji thamani madini ya Tanzania kwani alisema kuwa uongezaji thamani
madini ndani ya nchi utasaidia kuongeza ajira kwa wananchi, ubadilishanaji wa
teknolojia kutoka nchi zilizobobea katika shughuli hizo na kuwezesha ukusanyaji
wa kodi ambayo itasaidia katika shughuli nyingine za maendeleo.
Awali Meneja wa Kanzidata na Uchakataji wa
Taarifa za Jiolojia kutoka GST, Terence Ngole, alieleza JOGMEC na GST walisaini
Mkataba wa Makubaliano mwaka 2010 ambapo mashirikiano kati ya Taasisi hizo
yamesaidia kuongeza utaalam na teknolojia katika utafiti wa madini kupitia
mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na mfupi yanayotolewa na Shirika la JOGMEC.
Alisema kuwa Semina
hiyo imeshirikisha wadau mbalimbali kutoka Japan na Tanzania ambao
wanajishughulisha na Sekta ya Madini na Mazingira na kwamba ni semina ya kwanza
kuendeshwa nchini na Shirika la JOGMEC.
Post a Comment