Wakandarasi Wanaofunga Nyaya za Umeme Watakiwa na Kuwa na Kibali cha TANESCO
Na
Teresia Mhagama, Manyara
Wakandarasi wote wanaofanya kazi ya wanaofunga
nyaya za umeme ndani ya nyumba (wiring), wametakiwa
kuhakikisha kuwa hawafanyi kazi hiyo mpaka wawe wamepata idhini kutoka
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard
Kalemani wakati akiwa katika ziara ya
kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika wilaya ya Babati na
Mbulu mkoani Manyara.
“Baadhi ya Wakandarasi hawa wanaofanya wiring, wamekuwa wakitoza gharama kubwa
ya kutoa huduma hiyo na matokeo yake inapelekea wananchi kuchelewa kuunganishwa
na huduma ya umeme,” alisema Dkt Kalemani.
Aliongeza kuwa,
baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakifanya kazi hiyo chini ya viwango na
kupelekea matatizo mbalimbali kwa wananchi ikiwemo nyumba kupata hitilafu za
umeme na kusababisha majanga kama ya moto na kusisitiza kuwa yeyote
atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wakati huohuo, Dkt. Kalemani aliwaagiza Watendaji
wa TANESCO kutoa elimu kwa wananchi
kuhusu faida ya kutumia kifaa kijulikanacho kama UMETA (Umeme Tayari)
ambacho huwasha umeme ndani ya nyumba
bila mteja kulazimika kuingia gharama za kufunga nyaya za umeme ndani ya
nyumba.
“Kifaa hiki gharama yake ni shilingi 36,000
tu na kinaweza kutumika kwenye nyumba ya
chumba kimoja hadi vitano hivyo TANESCO mnapaswa kutoa elimu kwa wananchi ili
wakitumie kifaa hiki,”alisema Dkt.Kalemani.
Kuhusu miradi ya usambazaji umeme vijijini Awamu
ya Pili inayokamilika Oktoba 15, 2016, Mhandisi Mushi alisema kuwa miradi hiyo
itanufaisha vijiji 96 ambapo wilaya ya Babati
itakuwa na vijiji 56 vitakavyounganishwa na huduma ya umeme, wilaya ya
Mbulu itakuwa na vijiji 7, Hanang Vijiji 8 na Simanjiro ni vijiji 15.
Kuhusu vijiji ambavyo havijapata umeme katika
Awamu hiyo ya Pili, Dkt Kalemani alisema kuwa vijiji vyote ambavyo havina
umeme nchini vitaunganishiwa umeme
kupitia miradi ya REA ya Awamu ya Tatu ambayo utekelezaji wake utaanza mwishoni
mwa mwaka huu.
Post a Comment