Septemba 21,2016.
Na Genofeva Matemu – WHUSM
Serikali ipo tayari kuendeleza michezo yote badala ya kubaki na michezo michache ikiwemo mchezo wa mpira wa magongo (Hockey) ambao kwa miaka mingi iliyopita mchezo huo uliiletea heshima kubwa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye wakati wa ziara ya marais wa shirikisho la Mchezo wa Mpira wa Magongo Duniani na Afrika leo Jijini Dar es Salaam.
“Mchezo wa mpira wa magongo ni mchezo ambao Tanzania kwa miaka mingi iliyopita ulituletea heshima kubwa hivyo kwa ujio ziara ya marais wa shirikisho la Mpira wa Magongo (Hockey) Duniani na Afrika itasaidia kuurejesha mchezo huo kwenye hadhi yake”, alisema Mhe. Nnauye.
Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa Mchezo wa Mpira wa Magongo (Hockey) ni moja ya michezo ambayo inachezwa sana kwenye mishindano ya Olympic hivyo kama Tanzania itafanya maandalizi ya kutosha pengine Olympic ijayo ikapata fursa ya kuwa na wachezaji wa Hockey ambao watashiriki Olympic na kuiwezesha kupata medali za mchezo huo.
Naye Rais wa mchezo wa Mpira wa Magongo (Hockey) Duniani Bw. Leandro Negre ameahidi kusaidia miundombinu ya mchezo huo hasa uwanja kurejesha jitihada zinazofanywa na Tanzania huku akiiomba serikali kuipatia ardhi itakayowawezesha kujenga uwanja mzuri na wa kisasa kupitia shirikisho la mchezo wa mpira wa magongo duniani.
Aidha Rais wa Mchezo wa Mpira wa Magongo (Hockey) Afrika Bw. Seif Ahmed ameahidi kuongeza miundombinu katika uwanja wa kisasa utakaojengwa na shirikisho la mchezo wa mpira wa magongo duniani nchini Tanzania kwa kuuwekea miundombinu muhimu ikiwemo mataa na vitu vingine ili kuhakikisha uwanja huo unakua na hadhi ya kuchezwa michezo ya kimataifa.
Post a Comment