Tume ya Uchaguzi ( NEC ) yazindua Programu ya Utoaji Elimu ya Mpiga Kura Kwa Wananfunzi
Mkurugenzi Idara ya
Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel Kawishe
akitoa ufafanuzi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe nje
kidogo ya mji wa Musoma juu ya majukumu na utendaji wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wakati wa uzinduzi wa programu endelevu ya utoaji wa elimu ya mpiga
kura kwa kuyafikia makundi mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Idara
ya TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhandisi Manyiri Isaya akitoa ufafanuzi kwa
wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe nje kidogo ya mji wa
Musoma juu ya daftari la wapiga kura na namna taarifa za wapiga kura
zinavyotumika kwenye chaguzi mbalimbali. Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Huduma za
Kisheria wa NEC, Bw. Emmanuel Kawishe.
Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura wa NEC, Bi. Giveness
Aswile akiwaeleza wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe Musoma mfumo unaotumiwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) katika kuwawezesha watu walio katika makundi maalum hasa watu
wenye ulemavu wenye sifa kupiga kura
kupitia karatasi maalum.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Songe iliyoko nje
kidogo ya mji wa Musoma wakionesha vipeperushi na machapisho mbalimbali
waliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa lengo la kuwawezesha kuongeza
uelewa juu ya majukumu ya Tume wakati wa uzinduzi wa program endelevu ya utoaji
wa elimu ya mpiga kura mjini Musoma.
Mwanafunzi wa kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya
Songe, Musoma akiwauliza swali Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (hawapo
pichani) juu ya matumizi ya TEHAMA katika kuwabaini wananchi waliojiandikisha
kwenye kituo cha kupigia kura zaidi ya kimoja.
Baadhi ya wananfunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana na Songe nje
kidogo ya mji wa Musoma, wakifuatilia kwa makini elimu ya Mpiga kura iliyokuwa
ikitolewa na Maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika shule hiyo
wakati wa uzinduzi wa program ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kwa wananchi.
Baadhi ya wananfunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana na Songe,
Musoma wakipitia machapisho mbalimbali
ya elimu ya Mpiga kura yaliyotolewa na Maofisa wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) katika shule hiyo wakati wa uzinduzi wa program ya utoaji wa
elimu ya mpiga kura kwa wananchi.
Na Aron Msigwa – NEC, Musoma.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezindua rasmi programu ya utoaji wa
Elimu endelevu ya mpiga kura nchini kwa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa shule
ya Sekondari ya wasichana ya Songe iliyoko nje kidogo ya Manispaa ya Musoma
mkoani Mara.
Uzinduzi wa programu hiyo ni kuanza rasmi kwa mkakati wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata elimu ya mpiga kura ili kujenga
uelewa kuhusu majukumu ya Tume , utendaji wake
na uelewa wa chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini.
Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakati wa uzinduzi wa program
hiyo,
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
Bw. Emmanuel Kawishe amesema kuwa NEC imeamua kuwafikia moja kwa moja wanachi
ili iwapatie elimu kuhusu haki na wajibu walio nao kikatiba pia kuwajengea uelewa
wa kutosha kuhusu taratibu zinazosimamia chaguzi nchini.
Amesema kuwa programu
hiyo imezinduliwa kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu utendaji wa Tume na
kazi za Tume ili kuongeza uelewa miongoni mwa jamii pia kuiwezesha Tume hiyo kupokea
ushauri na maoni ya wananchi.
Bw. Kawishe ameeleza
kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inalojukumu la kutoa elimu ya mpiga kura
kwa mujibu wa Sheria kama ilivyoanishwa katika kifungu Na 4 (c) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 na kuongeza kuwa
imeanza kuwafikishia elimu ya mpiga wananchi kura moja kwa moja katika maeneo
yao.
Amesisitiza kuwa NEC imezindua programu hiyo katika shule ya Sekondari
ya wasichana ya Songe ili kuwapatia fursa vijana waliotimiza umri wa kupiga
kura na wale ambao bado hawajatimiza umri huo kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu
chaguzi zijazo.
Aidha, amewaeleza wanafunzi hao kuwa ili mwananchi aweze kupiga kura lazima awe amekidhi sifa na vigezo
vilivyoainishwa kisheria ikiwemo kutimiza umri wa miaka 18 na kuendelea, kupiga
kura katika kituo alichojiandikishia kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu
cha 63, kuwa na utimamu wa akili, kuwa na uraia wa Tanzania na vigezo vingine
vilivyoainishwa kisheria.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Idara ya TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mhandisi Manyiri Isaya akitoa
ufafanuzi kuhusu matumizi ya TEHAMA katika kuhifadhi na kutoa taarifa za wapiga kura waliojiandikisha katika daftari
la kudumu la wapiga kura ameeleza kuwa matumizi ya TEHAMA yamerahisisha utunzaji wa taarifa za wapiga kura na kufafanua kuwa mwananchi
aliyejiandikisha kwenye kituo kimoja cha kupigia kura hawezi kwenda kupiga kura
katika kituo kingine.
“Napenda ifahamike
kwamba kujiandikisha kwenye kituo zaidi ya kimoja kwa lengo la kupigia kura mara
nyingi ni kosa kisheria na mtu huyo anashitakiwa kwa mujibu wa sheria, Tume
tuna daftari la kudumu la wapiga kura tunapochakata taarifa za wapiga kura huwa
tunagundua watu waliojiandikisha zaidi ya kituo kimoja, tunachofanya sisi
tunachukua taarifa za kituo cha mwisho mtu alichojiandikisha” Amesisitiza.
Mhandisi Manyiri amefafanua
kuwa karatasi za kupigia kura hutolewa kulingana na idadi ya wapiga kura
waliojiandikisha katika kituo husika hivyo hakuna namna ambayo mwananchi anaweza
kupiga kura kwenye kituo zaidi ya kimoja.
Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura Bi. Giveness Aswile
akitoa ufafanuzi kuhusu wajibu wa Tume katika kushughulikia watu wenye mahitaji
maalum hasa watu wenye ulemavu ambao wanaokidhi sifa za kupiga kura amesema
kuwa Tume imekuwa ikiweka mazingira rafiki ya kuwawezesha kupiga kura.
Amesema kuwa katika uchaguzi
uliofanyika Oktoba, 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliandaa karatasi maalum za
kupigia kura na maeneo wezeshi ya kupigia kura ili kuwawezesha wananchi hao
kutumia haki yao ya Kikatiba kuwachagua viongozi wanaowataka.
“ Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika uchaguzi uliopita tuliweka mazingira
mazuri kwa watu wenye ulemavu, na wale wasioona ambao wana uwezo wa kusoma na
kuandika tukawawekea vifaa na karatasi maalum zenye nukta nundu ambazo zina
majina ya wagombea wa vyama vyote ili kuwawezesha kupiga kura wao wenyewe bila
msaada wa mtu yeyote” Amesisitiza Bi. Aswile.
Ameongeza kuwa NEC imekuwa ikitoa kipaumbele kwa makundi mengine hasa
ya wazee, mama wajawazito kupata huduma haraka katika vituo vya kujiandikishia
na kupiga kura bila kupanga mstari kama ilivyo kwa wananchi wengine.
Kwa upande wao walimu na wanafunzi wa shule hiyo wakizungumza kwa
nyakati tofauti kuhusu uzinduzi wa program hiyo katika shule yao wameishukuru
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuichagua shule hiyo kuwa ya kwanza kupata elimu
ya mpiga kura.
Wamesema kuwa elimu ya mpiga kura waliyoipata kupitia kwa maofisa wa
Tume na majibu ya maswali waliyouliza imewaongezea ufahamu na kuwajengea uwezo
wa kuwaelimisha vijana wengine kuhusu majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na
wajibu wao katika kushiriki kwenye chaguzi zijazo.
Wameiomba NEC iendelea kuwapatia vijana wengi zaidi elimu ya mpiga ili waweze kujitambua kuwa na uelewa sahihi juu ya majukumu na utendaji wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi.
Post a Comment