Washiriki wa Semina ya
26 ya Wabunifu majengo na Wakadiriaji majenzi wakimsiliza Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, (hayupo pichani) wakati wa
semina hiyo jijini Dar es salaam.
..................
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa Wabunifu
Majengo na Wakadiriaji Majenzi kuungana ili waweze kupata fursa katika miradi
mikubwa ya ujenzi itakayoanza hivi karibuni hapa nchini.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa semina endelevu ya 26 ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi,
Prof. Mbarawa amesema Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika ujenzi wa
miundombinu ya kisasa na itatoa kipaumbele kwa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji
Majenzi watakaoungana ili kuwa na nguvu ya kutekeleza miradi hiyo kwa viwango.
“Tunao mradi wa ujenzi
wa reli ya kisasa, ujenzi wa miundombinu ya kisasa mjini Dodoma, ujenzi wa
makazi ya kisasa ya wananchi, vyote hivi vinahitaji wataalamu walioungana,
wenye nguvu ya kufanya kazi kwa haraka na ubora unaokubalika”, amesisitiza
Prof. Mbarawa.
Ameitaka Bodi ya Usajili
ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kujitangaza na kuwatangaza
wataalamu wake ili huduma zao zitumiwe na wananchi wa ngazi zote kwa gharama
nafuu.
“Shirikianeni na vyuo
vinavyofundisha fani yenu ili viongeze udahili wa wanafunzi na kuhakikisha kazi
zenu zinafanywa kisasa na kwa kuzingatia teknolojia”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameitaka
Bodi hiyo kutoa elimu ya kutosha ili kuvutia wanafunzi wengi kupenda kusoma
fani hiyo na wale wanaofanya vizuri wawape motisha ya kuwasomesha katika vyuo
vikuu vya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika
semina hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya AQRB, Mbunifu Majengo Ambwene Mwakyusa,
amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Bodi yake imejipanga kuhakikisha wananchi
wanapata ramani za nyumba kwa bei nafuu ili kuwa na jamii yenye makazi ya
kisasa.
Naye Msajili wa Bodi
ya AQRB, Mbunifu Majengo Jehad Jehad amesema takribani Wabunifu majengo na Wakadiriaji
majenzi 1,333 pamoja na kampuni za fani hiyo 372 zimesajiliwa na zinatoa huduma
kwa mujibu wa sheria za fani hiyo.
Amebainisha kuwa Bodi
yake imejipanga kuhakikisha maadili ya taaluma hiyo hapa nchini yanalindwa na
atakayekiuka atafutiwa usajili na kuadhibiwa kwa mujibu wa taratibu ya bodi
hiyo.
Zaidi ya miradi ya
ujenzi 1,963 imekaguliwa na bodi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini katika
kipindi cha mwaka wa 2015 lengo ikiwa ni kuhakikisha ujenzi wowote unaofanyika
nchini unakuwa na viwango bora.
|
Post a Comment