Taasisi ya ADLG yaeleza Sababu ya Vijiji vinavyozunguukwa na Migodi ya Madini Kuwa Masikini
Taasisi ya Demokrasia na Utawala bora nchini ADLG, imebainisha kwamba kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa baadhi ya viongozi, kunasababisha maendeleo duni kwenye baadhi ya maeneo/vijiji yenye wawekezaji ikiwemo migodi.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Jimmy Luhende, ameyasema hayo leo kwenye mdahalo wa kila mwezi unaoendeshwa na taasisi hiyo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu rasilimali asilia ikiwemo madini, gesi na mafuta.
Amesema katika tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo katika vijiji mbalimbali vinavyozungukwa na migodi katika mikoa ya kanda ya ziwa, wamebaini kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii ikiwemo zahanati, shule, miundombinu bora ya barabara pamoja na maji safi na salama.
Amesema taasisi hiyo imeanzisha midahalo mbalimbali inayowahusisha wananchi pamoja na viongozi katika vijiji 147 vya mikoa minne ya kanda ya ziwa yenye uwekezaji wa madini ili kuwajengea uwezo wananchi kutumia uwekezaji ulio kwenye maeneo yao kurahishisha maendeleo.
Afisa Miradi (Sheria na Mikataba) kutoka taasisi ya ADLG, Carolina Tizeba, amesema katika tafiti zilizofanywa na taasisi hiyo kwenye Vijiji vinne vya Nyenze, Ikonongo, Songwa na Maganzo katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, umebaini kuwepo kwa ushiriki mdogo wa wananchi pamoja na uwajibikaji wa viongozi wao katika masuala ya uwekezaji wa madini jambo ambalo linasababisha kushindwa kufuatilia manufaa ya uwekezaji katika vijiji vyao na hivyo kuchangia kuwepo kwa huduma duni za kijamii katika vijiji hivyo ambavyo kuna wawekezaji wa madini.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Jimmy Luhende, akizungumza jambo kwenye mdahalo huo uliofanyika Isamilo Jijini Mwanza.
Nicholaus Ngelea ambaye ni Afisa Miradi ADLD, akiwasilisha mada kwenye mdahalo huo uliofanyika Isamilo Jijini Mwanza.
Carolina Tizeba ambaye ni Afisa Miradi (Sheria na Mikataba) ADLG, akiwasilisha taarifa ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwenye vijiji vinavyozungukwa na migodi mkoani Shinyanga.
Post a Comment