Shule nne za Wilayani Geita zapigwa "Tafu" ya Madawati na Tigo Fiesta 2016
Kampuni ya Tigo Tanzania leo imekabidhi madawati 185 yenye thamani ya shilingi milioni 31 yatakayogawiwa shule nne katika mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya mkakati wake unaoendelea nchi nzima wa kutoa msaada wa madawati ambayo yatainufaisha mikoa 14 bega kwa bega na tamasha la Tigo FIESTA 2016.
Mkakati wa kutoa msaada wa madawati katika msimo huu wa Fiesta unajulikana, “‘Dawati kwa kila mwanafunzi ni msingi wa elimu bora; Fiesta 2016 kwa Kishindo cha Tigo Elimu bora, Imooooo!’
Akizungumza katika sherehe za kukabidhi madawati hayo zilizofanyika katika Shule ya Msingi Mwatulole, Meneja wa Kikanda wa Tigo Kanda ya Ziwa Edgar Mapande, alisema umekuwepo uhitaji mkubwa wa madawati katika shule za msingi na kutokana na kuwepo kwa uhaba wa madawati imebainika kuwa ni moja ya sababu zinazoathiri uwezo wa kujifunza pamoja na ufanisi wa masomo miongoni mwa wanafunzi katika shule zetu nyingi za msingi.
“Lengo letu kama kampuni ni kuhakikisha kuwa tunaboresha mazingira ya kujifunzia katika shule zetu za msingi na tunayo furaha kwamba msimu wa FIESTA 2016 unaleta mabadiliko kwa kizazi cha baadaye ambacho ni wanafunzi walio katika shule za msingi kwa kuhakikisha hawakai tena chini sakafuni,” alisema Mapande.
Makabidhiano ya madawati hayo yalishuhudiwa na Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyingu ambaye alisema kuwa madawati hayo 185 yataboresha kwa kiwango kikubwa mazingira ya kujifunza kwa watoto katika mkoa huo na kutoa witom kwa watu wengine wenye mapenzi mema kujitokeza na kujiunga na juhudi hizo za kuondoa uhaba wa madawati uliobakia katika mashule mkoani humo.
Kyingu alizitaja shule zitakazonufaika na madawati hayo na idadi yake katika mabano kuwa ni Mwatulole (50), Nyankumbu (45), Ukombozi (45), na Kivukoni (45).
“Tunawashukuru sana Tigo kwa kutuunga mkono katika juhudi zetu kwa kupunguza idadi ya uhaba wa madawati katika shule za msingi mkoani Geita. Tunaamini madawati haya 185 yatatufikisha mbali katika kuwawezesha mamia ya watoto kuwa katika mazingira mazuri ya kujifunzia yanayotakiwa kwa ajili ya mafanikio katika kuelekea kuwa viongozi wa baadaye,” alisema Kyingu.
Mradi mkakati wa madawati wa Tigo Fiesta ulianzia mkoani Mwanza na hadi sasa Tigo imeshatoa madawati wilayani Kahama na mkoani Kagera.
Post a Comment