Waziri ABDALLAH POSSI aiwakilisha Afrika Mkutano wa Kutokomeza Umasikini
Na Mwandishi Maalumu
Siku ya tarehe 15 Juni, 2016, Mhe. Dkt. Abdallah Possi (MB),
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu alishiriki katika Mjadala wa
kutokomeza umasikini na kuleta usawa kwa watu wenye ulemavu.
Majadiliano hayo
yalikuwa ni moja ya mikutano muhimu iliyolifanyika katika Mkutano wa 9 wa nchi
ambazo zimeridhia Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu uliofanyika New York,
Marekani.
Mwenyekiti wa majadiliano hayo alikuwa ni Bi. Ellen Maduhu,
Afisa katika ofisi ya uwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa
ambaye pia ni Makamu wa Raisi wa Kamati ya Mkutano wa Nchi ambazo zimeridhia
Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (Vice President of the Conference of
State Parties to the Convention on the Rights of Persons of Disabilities).
Mhe. Dkt. Possi alikuwa ni mmoja wa watoa mada aliyeliwakilisha
bara la Afrika. Katika majadiliano hayo kulikuwa na watoa mada wengine
watano kutoka mataifa mengine wakiwemo Ms. Asa Regner, Waziri wa watoto,
wazee na usawa wa kijinsia kutoka Sweden; Bw. Joelson Dias, mjumbe wa Kamati
maalumu inayoshughulikia haki za watu wenye ulemavu, Brazil; Bi. Silvia
Quan kutoka Taasisi ya Haki za Binadamu wakiwemo watu wenye ulemavu,
Brazil; Ms. Mercedes Juan, kutoka Kamisheni ya Taifa kwa ajili ya maendeleo na
ujumuishwaji wa wenye ulemavu, Mexico; na Bi. Emi Aizawa kutoka Taasisi ya
Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) .
Katika Majadiliano hayo, watoa mada walilenga hoja zao katika
kujibu maswali ya mambo makuu matatu.
Jambo la kwanza lilikuwa kuelewa hatua zilizochukuliwa na
nchi husika na wadau wengine kupunguza umaskini na kukosekana kwa usawa
kwa watu wenye ulemavu.
Jambo la pili lilikuwa kujua hatua zilizochukuliwa na nchi
husika na wadau wengine katika kuhakikisha masuala muhimu ya watu wenye
ulemavu yanaingizwa katika sera zao za kitaifa za maendeleo na mipango ya
kuondoa umasikini na kuhakikisha usawa katika jamii.
Baadhi
ya Wajumbe wa Mkutano wa 9 wa nchi ambazo
zimeridhia Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wakifuatilia mada wakati wa
mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Umoja wa Mataifa New York Marekani Juni
15, 2016.
|
Suala la tatu lilikuwa kuelewa hatua zilizochukuliwa na wadau
mbalimbali katika kuhakikisha kwamba mipango ya maendeleo endelevu ya ajenda
2030 yanajumuisha masuala muhimu ya kuwakomboa watu wenye ulemavu kwa kuwaletea
maendeleo na usawa.
Katika mada yake, Mhe. Dkt. Possi alieleza kuwa katika
kuhakikisha Tanzania inatoa haki na usawa kwa watu wenye ulumavu, Serikali
imetengeneza sheria, sera na miongozo mizuri ya kusimamia usawa miongoni mwa
watu wenye ulemavu.
Alibainisha kuwa sera na Sheria nzuri zilizopo zinakabiliwa na
changamoto mbali mbali katika utekelezaji wake ikiwa ni pamoja na changamoto za
kiuchumi. Hata hivyo, Serikali imejipanga kukabiliana na changamoto hizo.
Vile vile Mhe. Possi alieza kuwa uchumi duni katika nchi nyingi
zinazoendelea umekuwa chanzo kikubwa cha kudhoofisha jitihada za kuleta maisha
bora kwa watu wenye ulemavu.
"Tanzania, kama mataifa mengine yanayoendelea, inakabiliwa
na changamoto za kiuchumi ambazo zinaathiri maisha ya watu wenye ulemavu, kama
vile upatikanaji wa maji safi, chakula, afya na elimu. Pia kuna tatizo la jumla
la ukosefu wa ajira, ambayo pia huathiri watu wenye ulemavu", alieleza
Mhe. Possi.
Dkt. Possi pia aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa mitazamo
hasi ya kijamii, na ukosefu wa vifaa muhumu vya kuwasaidia watu wenye ulemavu (assistive devices) vinachangia
kwa kiasi kikubwa kwa watu wenye ulemavu kutoshirikishwa katika masuala
ya jamii ikiwa ni pamoja na shughuli za kiuchumi.
Tatizo la upatikanaji wa vifaa kwa watu wenye ulemavu
limekwamisha maendeleo na ustawi bora wa watu wenye ulemavu hapa nchini,
hususani kwa wale wenye kipato cha chini.
"Kikwazo kikubwa kwa Tanzania ni ukosefu wa vifaa saidizi
kwa watu wenye ulemavu, hali hii inazuia Watu wenye Ulemavu kuendelea, kwa
sababu bila ya vifaa saidizi, Watu Wenye Ulemavu hawawezi kupata huduma
muhimu za kijamii kama elimu na mafunzo kwa ajili ya maisha ya kujitegemea na
mchango wa mchakato wa maendeleo wa taifa lao.
Hii inajenga kikwazo kingine cha
ajira na bila kuwa na ajira yenye kipato, watu wenye ulemavu wataendelea kubaki
maskini," alisisitiza Dkt. Possi.
Mwisho, Dkt. Possi alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa
kuzisaidia nchi kama Tanzania katika kupata vifaa saidizi vya watu wenye
ulemavu, ikibidi kupata teknolojia ya kuvitengeneza vifaa hivyo ndani ya nchi
ili vipatikane kwa urahisi.
Post a Comment