Serikali Kukarabati Uwanja wa Ndege wa MTWARA
Serikali kupitia Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imetenga shilingi bilioni 10 katika
mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa
Mtwara.
Hayo yamebainishwa na Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Edwin Ngonyani leo
Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini Mhe.
Hawa Ghasia lililohoji kuhusu ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara.
Mhe. Ngonyani alisema kuwa
Serikali imeendelea kufanya matengenezo ya mara kwa mara katika uwanja
huo na TAA inafanya tathmini ya uchakavu wa matabaka ya lami (Pavement
Evaluation) ya njia ya kuruka na kutua ndege ili kubaini ukarabati
stahiki unaotakiwa na matumizi ya fedha zinazohitajika na kazi hiyo ya
tathmini inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2016.
Aidha, Mhe. Ngonyani alieleza
kuwa katika mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja
vya Ndege inaandaa Mpango Kabambe (Master Plan & Concept Design) kwa
ajili ya ukarabati na upanuzi wa uwanja huo kutoka daraja 3C la sasa
kwenda daraja la 4E ili kuweza kuhudumia ndege kubwa zaidi hivyo kuwa
kitovu cha usafiri wa anga kwa Ukanda wa Kusini.
“Ukarabati na upanuzi wa uwanja
utahusisha miundombinu yote ya kiwanja ikiwemo taa na mitambo ya
kuongozea ndege pamoja na majengo. Kazi hiyo ya uandaaji wa Mpango
Kabambe na Usanifu wa Awali inatarajiwa kukamilika Julai 2016.” Alisema
Ngonyani.
Ikiwa ni mpango wa muda mfupi,
Mhe. Ngonyani aliongeza kuwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imeingia
makubaliano na Kampuni ya British Gas (BG) kwa ajili ya kutumia taa zake
ambazo ni za kuhamisha kwa ajili ya kuongozea ndege pale ambapo ndege
itatakiwa kutua usiku katika uwanja huo.
Post a Comment