Header Ads

Manispaa ya Kinondoni yawaagiza Walipa Kodi na Ushuru Kudai Stakabadhi za Kielektroniki

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni amewataka walipa kodi na ushuru katika Manispaa hiyo kudai stakabadhi za kielektroniki baada ya kufanya malipo ili kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya njia wanazozitumia katika ukusanyaji wa ushuru wa Manispaa hiyo.

“Napenda kuwasisitiza wananchi kuwa unapofanya malipo yoyote ya Manispaa lazima uhakikishe unapewa stakabadhi ya kielekroniki na iwapo hutopewa, unaruhusiwa kutoa taarifa kwa kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi kwenda 0767643460 na utapatiwa maelekezo ya nini cha kufanya”,alisema Kagurumjuli.

Kagurumjuli ameongeza kuwa Ofisa yeyote atakayekaidi kutoa stakabadhi hizo atachukuliwa hatua kali za kisheria kwani kukwepa kulipa mapato ni kurudisha nyuma uchumi wa nchi.

Aidha, Mkurugenzi huyo ameyataja maeneo ambayo mwananchi anaweza kulipia kodi au ushuru na kupata stakabadhi za kielekroniki ni Ofisi za Manispaa, Ofisi za Kata, Benki ya CRDB pamoja na watumishi wa Manispaa waliopo katika shughuli maalumu za ufuatiliaji wa kodi na ushuru.

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilianza kutumia mfumo wa kulipa kodi na ushuru kwa njia ya kielekroniki mnamo mwaka 2013 , na mwaka 2015 ilipata tuzo ya ukusanyaji bora wa mapato kwa njia hiyo kwa Tanzania na Afrika nzima.

No comments

Powered by Blogger.