Kongamano la Uadilifu na Utawala Bora lafanyika Chuo cha Mwalimu NYERERE
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk.Lenard Akwilapo akikabidhiwa picha na Mwakilishi Makazi wa Shirika la KAS, Daniel El-Noshokaty ya waasisi wa ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika lisilo la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) la nchini Ujerumani, Hayati Mwalimu Julius Nyerere (kushoto pichani) na Konrad Adenauer (kulia), wakati wa Kongamano la la kitaifa na kimataifa lililokuwa na mada yake kuu uadilifu wa viongozi na utawala bora katika usimamizi wa maliasili kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Tanzania lililofanyija katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni Dar es Salaam juzi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara, Philip Mangula akichangia jambo kwenye kongamano hilo.
Taswira katika ukumbi wakati wa kongamano hilo.
Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Apium Chengula (kulia), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akitoa majumuisho yaliyofikiwa katika kongamano hilo.Kushoto ni Mratibu wa Mipango wa Shirika la KAS, Richard Shaba.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk.Lenard Akwilapo (katikati mbele waliokaa), akiwa na viongozi mbalimbali na wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere wakati wa kongamano hilo. Kutoka kulia waliokaa ni Mratibu wa Mipango wa Shirika la KAS, Richard Shaba, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara, Philip Mangula, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk. Shadrack Mwakalila, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la KAS, Daniel El-Noshokaty, Naibu Mkuu wa Chuo Utawala Fedha na Mipango, Dk. Margaret Shawa na Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Dk. Thomas Ndaluka.
Na Dotto Mwaibale
VYOMBO vyenye mamlaka vimetakiwa visiwatishe waandishi wa habari pale wanapo andika habari sahihi za kuikosoa serikali nchini badala yake viwalinde.
Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Apium Chengula wakati wa majumuisho yaliyofikiwa katika kongamano la kitaifa na kimataifa lililokuwa na mada yake kuu uadilifu wa viongozi na utawala bora katika usimamizi wa maliasili kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Tanzania.
"Tulipitisha maazimio kadhaa kama wenye mamlaka kuvilinda vyombo vya habari vinapo andika habari sahihi za kuiokosoa serikali, kuhimiza viongozi kuzingatia maadili na kupata mafunzo ya uongozi, kuhimiza viongozi kulinda maliasili ambazo ni endelevu na kusisitiza kuwa na itikadi inayoeleweka katika kuongoza nchi" alisema Chengula.
Kongamano hilo liliandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni kwa ufadhili wa Shirika lisilo la kiserikali la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) la nchini Ujerumani.
Chengula alisema kongamano hilo lilifanikiwa kutokana na kuwa na mada moto moto zilizohusu rasilimali za taifa na suala zima la utawala bora na kuwa lilisimamiwa na Kibweta cha Mwalimu Nyerere.
Alisema Kibweta cha Mwalimu Nyerere ni idara iliyoanzishwa chuoni hapo kwa ajili ya kusimamia masuala yote ya mafunzo ya viongozi na maadili ya viongozi iliyoanzishwa mapema mwaka jana na kuzinduliwa na Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete.
"Katika kongamano hilo kuliwa na mada mbalimbali zilihusu maliasili za Tanzania na jinsi zinavyo wasaidia wananchi ambayo ilitolewa na Profesa Aidan Msafiri kutoka Chuo cha Kanisa Katoliki Mwenge, mada nyingine ikiwa ni utawala bora kuhusu mali asili changamoto na fursa zake iliyoendeshwa na Dk.Camirius Kasala kutoka Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki na kuwa mada ya tatu ilihusu maendeleo endelevu katika Tanzania mchango wa utawala bora unaozingatia maadili ya uongozi bora" alisema.
Alisema Hayati Mwalimu Julius Nyerere kabla ya Uhuru 1961 alikwenda nchini Ujerumani ambapo alionana na Muasisi wa Shirika la KAS, Konrad Adenauer na kuona ni jinsi gani wataweza kusaidia kutoka mafunzo ya uadilifu kwa viongozi na tangu hapo walianzisha ushirikiano huo ambao unaendelezwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Shirika hilo ambalo limefanikisha kudhamini kongamano hilo.
Post a Comment