Wataalam wa Takwimu Barani Afrika Wakutana Jijini DAR ES SALAAM
Na Emmanuel Ghula, Dar es Salaam
VIONGOZI wa Ofisi za
Takwimu barani Afrika leo wamekutana kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi
hizo pamoja na Uboreshaji wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu katika
nchi za Afrika.
Wakizungumza katika mkutano
wa wataalam wa takwimu ulioanza leo Jijini Dar es Salaam, viongozi hao wamesema
ili takwimu bora zipatikane kwa wakati, ni lazima kuwepo na mfumo bora wa uongozi
pamoja na wataalamu waliobobea katika fani ya takwimu.
Akizungumza katika
mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amesema
lengo la mkutano huo ni kujadili mfumo wa uongozi bora katika Ofisi za Takwimu
pamoja na namna ya kuboresha mitaala ya ufundishaji wa masomo ya takwimu barani
Afrika.
“Leo tupo hapa
wataalamu wa takwimu kutoka zaidi ya mataifa 25 barani Afrika ili kujadili
namna ya kuboresha mifumo yetu ya uongozi katika Ofisi za Takwimu pamoja na
kujadili mbinu bora za kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa watakwimu vijana hasa
kupitia upya mitaala ya ufundishaji,” amesema Dkt. Chuwa.
Dkt. Chuwa amesema kuimarishwa
kwa mfumo wa uongozi pamoja na kuboresha mafunzo kwa wakwimu kutasaidia katika ukusanyaji
wa takwimu bora zitakazotumika katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkuu Msaidizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu wa Afrika ya Kusini, Risega Maluleke
amesema mataifa mengi ya Afrika yanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na
uwezo wa kujitegemea kifedha kitu ambacho hukwamisha upatikanaji wa takwimu kwa
wakati.
Amesema licha ya
changamoto hiyo, kwa kiasi kikubwa kazi ya ukusanyaji wa takwimu imekuwa
ikifanyika kwa ufanisi mkubwa kutoka kwa watalaam hao wa takwimu na hivyo
kupitia mkutano huu, wataweza kujadili namna ya kuboresha uimarishaji wa Ofisi
za Takwimu.
Maluleke amesema ni vyema Serikali zikaziwezesha ofisi za
ukusanyaji wa takwimu ili ziweze kujitegemea kibajeti na kuboresha utendaji
kazi wake katika kuhakikisha takwimu bora zinapatikana kwa wakati muafaka.
Mkutano huo wa siku
tano unatarajia kumalizika tarehe 06 Novemba, 2015 ambapo wataalam takribani 30
wamekutana kujadili Mfumo wa Uongozi Bora katika Ofisi hizo pamoja na Uboreshaji
wa Mitaala ya Ufundishaji wa Masomo ya Takwimu katika nchi za Afrika.
Post a Comment