Header Ads

Bilioni 1.4 zachangwa na Mabalozi,Wafanyabiashara Kusaidia waathirika wa tetemeko Kagera

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza na Wafanyabiashara na Mabalozi (hawapo pichani) wakati wa uchangiaji wa waathirika wa tetemeko mkoani Kagera uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Na Sheila Simba, MAELEZO

Jumla ya shilingi bilioni 1.4 zimechangwa na mabalozi na wafanyabiashara kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera.

Michango hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam katika harambee iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na kufanyika Ikulu.

Akizungumza katika harambee hiyo Waziri Mkuu alisema jumla ya nyumba 840 zimebomoka na kuharibika kabisa, wakati nyumba 1264 zimepata hitilafu na zinaweza kufanyiwa marekebisho ili watu waendelee kuishi katika nyumba hizo.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa shule 4 za sekondari ambazo ni Nyakato, Ihungo, Kashange na Buhembe zimeharibika na mbili kati ya hizo yaani Ihungo na Nyakato zimefungwa  kutokana na kuharibika sana.

Madhara mengine yaliyosababishwa na tetemeko hilo kwa mujibu wa Waziri Mkuu ni kuharibika kwa vituo vya afya, miundombinu ya barabara, umeme na njia za mawasiliano na kufanya athari za tetemeko kuwa kubwa.
Mabalozi na wafanyabiashara mbalimbali wakimskiliza Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa (hayupo Pichani) wakati wa uchangiaji wa waathirika wa tetemeko mkoani Kagera uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni kumi  kutoka kwa katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Aziz Mlima wakati wa uchangiaji wa waathirika wa tetemeko mkoani Kagera uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Kutokana na athari hizo Waziri Mkuu amewaomba mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kusaidia waathirika kwani ni tukio ambalo halikutarajiwa na limeleta hasara kubwa kwa wanakagera na Taifa kwa ujumla.

“Licha ya michango hii ninayowaomba leo, tutaandaa safari kwa anayehitaji kwenda kujionea hali halisi ili aone ni namna gani atakavyosaidia,”alisema Waziri Mkuu.

Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kuwa imefunguliwa akaunti ya kuchangia katika maafa hayo kwenye benki ya CRDB inayojulikana kama KAMATI MAAFA KAGERA akaunti namba 0152225617300 na swift code ambayo ni CORUtztz na kuwaomba wananchi na watu wengine kutumia akaunti hiyo kwa kusudi hilo.

Majaliwa amesema pia kuwa utaratibu unaandaliwa ili kuwawezesha watu kuchangia kwa njia ya Mpesa, tigopesa na Airtelmoney. Utaratibu huo utakapokuwa tayari utatangazwa ili kuwarahisishia watumiaji wa mitandao hiyo kuchangia.

Tetemeko hilo la ardhi ni kubwa kuliko yote ambayo yamewahi kutokea hapa nchini na hadi sasa limesababisha vifo vya watu 17 na kuharibu nyumba, majengo na miundombinu mkoani Kagera.


No comments

Powered by Blogger.