Header Ads

Waraghbishi Wilayani KAHAMA wapania Kumkomboa Mwanamke


Na Krantz Mwantepele,Kahama

Wanawake ni nguzo muhimu sana katika uchumi wa watanzania wengi. Mwanamke ana ushawishi mkubwa na hasa pale anapoamua kuwa chachu ya maendeleo. Na hasa anapowezeshwa kufanya hivyo.

Katika kufanikisha hili waraghbishi wameamua kutoa mafunzo ya uraghbishi kwa makundi mengine ya jamii. Mojawapo ya kundi hilo ni la wanawake. Waraghbishi wapya toka katika kijiji cha Nyandekwa, kati ya hao wapo 9 ambao ni wanawake.

Mmoja wao ni Anna Alphonce, Mwenyekiti wa kitongoji cha Busolo, katika kijiji cha Nyandekwa. Akielezea jinsi alivyoanza uraghbishi alisema:

“Mi niliona kuna kikundi wanakaaga humu karibu kila jioni. Na kila nilipokuwa napita jirani na hapa naona watu wamejaa, basi nikapenda namimi nijiunge nao na hasa baada ya kujua nini wanafanya. Na hapo ndipo nilipoanza uraghbishi,”


Anna Alphonce (katikati) ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Busolo akifafanua jambo wakati akielezea uraghbishi anaofanya.
...........................

Akiwa kama mwenyekiti mwanamke wa kitongoji aliweza kutumia nafasi yake kufanya uraghbishi kwa anaowaongoza. Kwa kuwa kilikuwa ni kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu, aliitisha mikutano kwenye kitongoji chake kwa lengo la kutoa hamasa ya wananchi kujitokeza kwa wingi. 

Kwa nafasi yake aliweza kuyafikia makundi ya wazee, vijana na wanawake. Ingawa kati ya hawa wanawake ndio walikuwa washiriki wazuri.

“Msisitizo kwenye mikutano yangu ilikuwa ni kupiga kura kwa amani. Niliwasihi Vijana wetu wasiwe chanzo cha vurugu na badala yake wawe walinzi na kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya utulivu,”
Haya ni maelezo ya mwenyekiti huyo akielezea jinsi alivyotumia nafasi yake kwenye kufanya hamasa ya amani. Akaongeza,
“Kwangu mimi haya ni mafanikio kwa sababu kweli uchaguzi umefanyika kwa amani katika kitongoji change.”

Mraghabishi mwingine ni Matrida Peter toka katika kijiji cha Nyandekwa, yeye uraghbishi wake alifundishwa na Elizabeth Ngaljalina toka kijiji hicho hicho. Baada ya kufundishwa yeye alichoamua kufanya uraghbishi kwa vijana wa kijiji cha Nyandekwa pamoja na wale waliokuwa mashuleni pia.

Akielezea jinsi ambavyo anafanya uraghbishi kwa vijana, Matrida anasema,
“Nafundisha makuzi ya ujana ili kuweza kutimiza ndoto zao. Kwanza nawaelewesha kuhusu mabadiliko ya miili yao hasa wanapoingia hatua ya kubalehe na kuvunja ungo. Hii inawasaidia jinsi ya kujikinga na maambuzi ya virusi vya ukimwi.”

Uraghbishi wake hauishii kwa vijana walio nje ya shule, hivyo alikwenda kumtembelea ili aweze kupata fursa ya kutoa elimu hiyo hasa kwa wanafunzi ya shule ya msingi. Walengwa wakubwa wakiwa ni wanafunzi wa kuanzia darasa la nne mpaka la saba. 

Akielezea rika la watoto hao, Matrida anasema:

“Watoto wa siku hizi wana maumbo makubwa, hivyo hao wa darasa la nne mpaka la saba sio wadogo kiumbo na wengi ndio wapo kwenye huo umri. Wanahitaji mwongozo manake makuzi siku hizi yameachwa kwa wazazi na wao mda mwingine wanaona aibu kuongea nao,”
Matokeo ya uraghbishi huu wa mwanamama Matrida ni kuongeza kwa watoto wenye uelewa wa mipango ya uzazi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Kwani maambukizi katika wilaya ya Kahama yapo juu kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini.

Uraghbishi una maana tofauti tofauti kwa wanawake hawa wa kijiji cha Nyandekwa, 

kama anavyoelezea Mariam Stephano aliyeanza uraghbishi mwezi Septemba 2015:
“Uraghbishi kwangu mimi ni kutetea haki za vijana na mabinti, na sio tu kutetea bali kujua na falsafa yake ya jinsi ya kutenda ili kufanikisha lengo hilo ninaloliangalia kama  ndio jukumu langu,”
Wakati Suzan Stephano yeye analinganisha uraghbishi na haki za kikatiba. Huku akisisitiza umuhimu wa kuthaminiwa kwa mwanamke katika kijiji chao na taifa kwa ujumla. Na yeye pia anakiri kwa uraghbishi ni falsafa ya jinsi ya kutenda.

Waraghbishi wanawake toka katika kijiji cha Nyandekwa wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kitongoji cha Busola akielezea uraghbishi wake katika ngazi ya kitongoji
........................

Mraghbishi mwingine ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Bujika, Adam Joseph yeye alijiunga na uraghbishi mwezi Septemba 2015, kwa kutumia nafasi yake uwenyekiti alitambulisha uraghbishi kwenye kitongoji chake.

“Cha kwanza nilichofanya ni kuongea na mtendaji wa kijiji na kukubaliana tunahitaji kufanya hamasa kwa vijana ili wawe wanafika katika mikutano ya vijiji. Hivyo nikaanza kupita kwenye vijiwe na kuwahamasisha vijana waweze kufika mikutanoni. Na tuliwalenga vijana wote wa kike na wa kiume,” anaelezea Adam.

Vijana walimwambia mwenyekiti wao kwamba wao hawasikilizwagi wakija kwenye mikutano na hivyo hawaoni umuhimu wa kuja kwenye mikutano ya vijiji. Majibu haya yalimpelekea mwenyekiti kuitisha mkutano uliowausisha vijana na wazee kwa pamoja.

“Nimeshaitisha mikutano miwili, muamko bado si mkubwa sana kwani bado vijana hawaoni umuhimu wa kushiriki mikutano hii. Lakini hili halinikatishi tamaa najua hapa ni mwanzo tu,” anaelezea Adam.


Kwa hakika hizi ni harakati za kweli katika kumwezesha mwanamke na jamii kwa ujumla. Waraghbishi kwa pamoja wanakili kwamba uraghbishi ni falsafa ya kutenda. Swali la msingi kwetu sote, je na sisi tunatenda na kama ndio tunatumia falsafa gani.


                         

No comments

Powered by Blogger.