Serikali yapiga Marufuku Matumizi ya Barua Pepe za Kawaida Katika Mawasiliano yake
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe. Angella Kairuki (kushoto) akipokewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi
za Wakala hiyo jijini Dar es salaam.
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe. Angella Kairuki (katikati) akiwasili Ofisi za Wakala ya Serikali
Mtandao kwa ziara ya kikazi leo jijini Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe. Angella Kairuki (kushoto) kuhusu utendaji wa Wakala hiyo leo wakati
wa ziara ya kikazi ya Mhe. Angella
Kairuki katika Ofisi za Wakala hiyo leo jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Uratibu
wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wakala ya Serikali Mtandao Bw. Benjamin Dotto akitoa
ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais
Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) kuhusu kituo cha
ufuatiliaji mifumo ya mawasiliano Serikalini leo jijini Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. Angella Kairuki (kulia) kuhusu kituo cha ufuatiliaji mifumo ya mawasiliano
Serikalini leo jijini Dar es salaam.
aziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. Angella Kairuki (kulia) akitembelea maeneo mbalimbali ya Ofisi za Wakala
ya Serikali Mtandao leo. Katikati ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao
Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini
Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya
Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe. Angella Kairuki (anayefuatilia kushoto) kuhusu utendaji wa Wakala hiyo leo wakati
wa ziara ya kikazi ya Mhe. Angella
Kairuki katika Ofisi za Wakala hiyo leo jijini Dar es salaam.
Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala
Bora Mhe. Angella Kairuki akizungumza na Watendaji na baadhi ya Wafanyakazi wa
Wakala ya Serikali Mtandao leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za
Wakala hiyo jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa – Dar es salaam
Serikali imepiga marufuku matumizi ya Barua pepe za
kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea taarifa za Serikali na
kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo rasmi wa Mawasiliano ya
Barua Pepe Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha
mawasiliano kwa njia ya Mtandao.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angella
Kairuki alipokuwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wakala ya Serikali
Mtandao ( e Government Agency) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji na
ufanisi wa matumizi ya TEHAMA Serikalini.
“Sasa kuna watumishi 7000 wanaotumia anwani za Barua pepe za Serikali ,idadi hii ni ndogo lazima
iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za Serikali kwa
kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huu” Amesisitiza na
kuongeza kuwa Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye
mawasiliano binafsi.
Amesema kwa kutambua umuhimu
wa uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA Serikalini na kuongezeka kwa matumizi
ya TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao mbalimbali ipo haja ya kuweka
msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia Barua Pepe za Serikali.
Mhe. Kairuki amewataka watendaji wa Wakala hiyo
kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa Wizara,
Idara na Taasisi zote za umma zinaunganishwa
na mfumo rasmi wa Serikali ili kuwa na mfumo mmoja wa Mawasiliano.
“Katika hili ninatoa siku 60
muhakikishe kuwa mnakamilisha kwa Taasisi zilizobaki ili kwa wale watakaopuuzia
hatua zianze kuchukuliwa”
Ameeleza Mhe. Angella.
Aidha, ametoa wito kwa watendaji wa Wakala hiyo kuweka
mpango wa kuwawezesha na kuwajengea
uwezo wa kitaaluma watumishi waliopo kazini kwa kujenga utaratibu wa kuwarithisha uzoefu
watumishi ili kuendelea kuimarisha ufanisi na utendaji wa Wakala hiyo.
Mhe. Kairuki amewataka kuwa wabunifu katika kuanzisha
mifumo mipya ya TEHAMA ili kuimarisha
dhana ya Serikali mtandao ili kupunguza gharama
hadi kufikia asilimia 5 ya fedha zinazotumika kuendeshea masuala mbalimbali
ambayo yangefanywa kupitia matumizi ya TEHAMA.
Akizungumzia kuhusu ununuzi wa vifaa vya TEHAMA
serikalini ameitaka Wakala hiyo kutoa ushauri ili kudhibiti mianya ya
ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika
kununulia vifaa hivyo kwa gharama kubwa wakati vinaweza kupatikana kwa bei ya
kawaida.
“katika hili Serikali
itachukua hatua kwa yeote atakayebainika katika upotevu wa mapato muhakikise
mnazisaidia Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali katika masuala ya ununuzi
wa mifumo na vifaa vya TEHAMA ili mifumo inayonunuliwa iwe na manufaa kwa
wananchi na thamani halisi ya fedha”
Amesema Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa huduma
kupitia mtandao ili wananchi waweze kupata huduma hizo mahali walipo kwa gharama nafuu na kutoa wito
kwa watumishi wa Wakala ya Serikali mtandao (e-Gov) kuwa wabunifu katika kutengeneza programu
mbalimbali na mifumo salama itakayowasaidia wananchi kupata huduma.
Aidha, katika hatua nyingine ameitaka e-Gov kuendelelea
kujenga uwezo katika kudhibiti dharura na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza
katika matumizi ya TEHAMA na kuitaka Wakala hiyo iendelee kulifanyia kazi suala
la kuwezesha mifumo ya Serikali kuzungumza kati ya taasisi moja hadi nyingine
ili huduma zote ziweze kupatikana katika
eneo moja na kuondoa urudufu wa mifumo
iliyopo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali
Mtandao (e-Gov) Dkt. Jabiri Bakari akitoa taarifa ya utendaji wa Wakala hiyo
amesema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali toka kuanzishwa kwake
Julai 11, 2012 imeendelea kupata ufanisi katika uimarishaji wa Serikali
Mtandao.
Amesema kuwa Wakala hiyo inaendelea kuhakikisha kuwa
huduma za Serikali zinawafikia wananchi kupitia mtandao mahali walipo na
kuhakikisha kuwa inafanikisha lengo la huduma zote za Serikali kupatikana chini
ya dirisha moja.
Aidha amesema kuwa Wakala ya Serikali Mtandao
itaendelea kuhakikisha kuwa usimamizi wa viwango vya matumizi ya TEHAMA katika
Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali vinazingatiwa.
Post a Comment