Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Chafanya Mahafali ya Kwanza ya SHAHADA ya Takwimu Rasmi
Na Emmanuel Ghula –NBS
KATIBU Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue amevitaka vyuo na taasisi za elimu nchini kuhakikisha
vinatoa mafunzo bora yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Akizungumza jijini Dar
es Salaam katika mahafali ya kwanza ya Shahada ya Takwimu Rasmi katika Chuo Cha
Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC), Sefue amesema ni vyema vyuo na taasisi za
elimu kuhakikisha vinafanya tafiti kujua mahitaji ya wataalamu wanaotakiwa na
kutoa mafunzo yanayoendana na soko la ajira.
“Nchi yetu inahitaji
kuwa na watalaamu wa fani mbalimbali hivyo ni wajibu wa vyuo vya elimu ambavyo
ndio wazalishaji wa wataalamu hao kuhakikisha vinatoa wataalamu wenye ujuzi wa
kutosha unaoendana na mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi,” alisema
Sefue.
Sefue alisema kutokana
na umuhimu wa takwimu katika maendeleo, Serikali imekuwa mstari wa mbele
kupitia Wizara ya Fedha kuhakikisha inakisaidia chuo hicho kukabiliana na
changamoto zinazokikabili ikiwemo uhaba wa fedha za kuendeshea chuo hicho.
Aidha, alisema chuo
hicho kuanza kutoa shahada ni hatua kubwa kwasababu chuo hicho ndio tegemeo la Afrika katika kuzalisha
watakwimu wanaosaidia katika ukusanyaji wa takwimu bora zinazotumika katika
kupanga na kupima utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Aidha, Sefue amekitaka
chuo hicho kubuni miradi mbalimbali itakayosaidia kujipatia fedha kwa ajili ya
kutatua baadhi ya changamoto zinazojitokeza chuoni hapo.
Alisema Chuo Cha
Takwimu cha EASTC mwaka huu kimefikisha miaka hamsini ya utoaji wa mafunzo ya
Takwimu na wataalamu mbalimbali wa takwimu wanaofanya kazi Serikalini wamepitia
hapo na hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inakiendeleza ili kiwe kituo
bora zaidi kwa utoaji wa watakwimu waliobobea.
Kwa upande wake Mkuu
wa Chuo hicho, Professa Innocent Ngalinda amesema chuo hicho kimejipanga vyema
kuhakikisha kinaendelea kuzalisha watakwimu bora na wenye weledi katika fani ya
takwimu.
“Hivi sasa tumefikia
hatua kubwa sana ya kuanza kutoa wahitimu wa Shahada ya kwanza ya Takwimu
Rasmi, tutaendelea kuwa mhimili wa uzalishaji wa wataalamu hawa muhimu katika
maendeleo ya nchi yetu na bara la Afrika kwa ujumla,” alisema Professa
Ngalinda.
Professa Ngalinda
alisema chuo hicho kitaendelea kufanya kazi kwa karibu na nchi wanachama ili
kuhakikisha wahitimu wake wanakuwa chachu ya maendeleo kwa kusaidia ukusanyaji
wa takwimu bora na kwa wakati ili zitumike katika kupanga na kutekeleza mipango
mbalimbali ya maendeleo.
Jumla ya wanafunzi 29
wamehitimu na kutunukiwa Shahada ya kwanza ya Takwimu Rasmi katika mahafali hayo
ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika.
Post a Comment