Mawakili Wapashwa Kuzingatia Maadili ya Taaluma ya Sheria
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju (kulia) akiwasili katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam leo wakati wa hafla ya 53 ya kuwapokea na kuwaapisha Mawakili wapya 104. |
Mawakili wakiwa wamesimama mbele ya Jaji Mkuu kabla ya kuapishwa. |
Mawakili walioapishwa wakiwa katika picha
ya pamoja na Jaji Mkuu Mhe. Othman Chande na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania.
|
Na Aron Msigwa –MAELEZO
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Othman Chande amewataka Mawakili
kote nchini kufanya kazi zao kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma ya
Sheria na kwamba wasisite kuwaeleza ukweli wateja wao wanaopeleka mashauri
Mahakamani ili kuepuka kupoteza muda na gharama katika masuala yanayoweza
kupatiwa ufumbuzi nje ya Mahakama.
Akizungumza na Mawakili wapya 104 waliohitimu Shule ya
Sheria kwa mwaka 2015 wakati wa hafla ya
53 ya kuwapokea na kuwaapisha iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee leo
jijini Dar es salaam amesema kuwa msingi mkubwa wa kazi yao umejengwa katika
uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya sheria.
Amewataka Mawakili hao kubadilika kifikra kwa kuwa
Mawakili Bora ili kujenga imani na uaminifu kwa jamii wanayoihudumia na
kuongeza kuwa
sasa wameingia kwenye utaratibu wa kutambuliwa rasmi na
Mahakama ya Tanzania kwa kuwezeshwa kufanya shughuli za uwakili kwenye mahakama
ya Tanzania maeneo mbalimbali nchini.
“Naomba mtambue kuwa kila
Wakili ni Ofisa wa Mahakama hivyo mnao wajibu na jukumu la kusoma, kufuatilia
mashauri mbalimbali ili kuwa na uhakika wa kesi mnazosimamia kuliko kuzitegemea
Mahakama”
Aidha, ameeleza kuwa yapo mambo ambayo yamekua yakifanywa
na baadhi ya Mawakili wasio waaminifu yanayochafua sura ya Taaluma ya Sheria
ikiwemo kutumia nyaraka za kughushi, kuvunja Kanuni na Maadili ya Taaluma huku
baadhi yao wakijikuta wakiingia katika mgogoro na Mamlaka zinazosimamia kitaaluma
taaluma hiyo.
“Nawataka mzingatie sheria,
kanuni na Maadili ya Uwakili, hata hivyo tuna chombo kinachosimamia maadili
yenu, wapo takribani 176 waliokiuka maadili na hawa wanashughulikiwa kwa mujibu
wa Sheria ili kulinda maadili na utendaji wa taluma yenu” Amesisitiza Mhe. Othman.
Amewataka watimize
wajibu wao kwanza kwa wananchi watakaouhudumia pamoja na Mahakama ya Tanzania
ambayo inawataka kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Mhe. Othman amefafanua kuwa Mahakama ya Tanzania
inaendelea na Mkakati wa kupunguza mrundikano wa Kesi Mahakamani kwa
kuhakikisha kuwa kesi zote zinazofikishwa Mahakamani zinamalizika katika kipindi cha chini ya mwaka
1
Ameeleza kuwa silimia 47 ya kesi zaidi ya 200
zilizokuwepo Mahakama Kuu katika kipindi cha miaka 4 iliyopita zimeendelea
kusisikilizwa kwa ubora na sasa zimebaki asilimia 17 ya kesi hizo jambo
linaonyesha kuongezeka kwa ufanisi wa Mahakama.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe.
George Masaju akiwakaribisha Mawakili hao katika familia ya sheria Tanzania
amesema kuwa katika jamii wanao mchango mkubwa katika kuhakikisha Haki na Usawa
vinadumishwa nchini.
Amesema mawakili hao kabla ya kuapishwa na kuingizwa
kwenye utaratibu wa kutambuliwa kuwa Mawakili wamepitia na kufauru vigezo vya
kitaaluma vilivyowekwa ili kulinda heshima ya Taaluma ya sheria nchini.
Amewaeleza kuwa mara baada ya kupokea viapo vyao wameingia
kwenye utumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ya kikatiba na kuongeza kwamba
wao kama wanasheria wanatakiwa kuzingatia weledi wa taaluma yao.
Amewataka kuwa makini katika utendaji wao kwa kuepuka
kuwa sehemu ya migogoro na kuepuka kuegemea upande wowote watakapokuwa
wakitimiza majukumu yao ili kuendelea kujenga jamii ya kistaarabu na ya
kidemokrasia.
" Naomba mkumbuke kuwa mna wajibu mkubwa kwa watu
mtakaokuwa mnawahudumia, zingatieni maadili maana ninyi sasa ni sehemu ya
Mahakama ya Tanzania, fanyeni kazi kwa weledi na umakini mkubwa"
Amesisitiza.
Amesema utekelezaji wa majuku yao ya kila siku ni
sehemu ya utumishi wao katika umma hivyo wasiruhusu aina yoyote ya ukiukwaji wa
maadili yakitika kutimiza majukumu yao na kuwasaidia wananchi wasiokuwa na
kipato/ wananchi masikini watakakao omba msaada wao wa kisheria.
Aidha amewataka wawe wabunifu, kufanya kazi kwa bidii
na kujiendeleza pale inapowezekana ili waweze kuwa msaada kwa wananchi walio na
kiu ya kupata huduma kutoka kwao.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS) Charles Rwechungura akizungumza wakati wa wa kuwakaribisha
mawakili hao 134 amesema kuwa wao kama Chama cha Wanasheria wanayofuraha ya
kuwakaribisha wanachama wapya kwenye uwanja wa Sheria nchini.
Amesema mawakili hao wameingia katika wakati muafaka
kuongeza nguvu katika kuwahudumia wananchi huku akieleza kuwa shule ya
Wanasheria Tanzania itaendelea kutoa mafunzo na kusimamia viwango vya taaluma
ya sheria nchini na kuwataka mawakili hao kulinda heshima ya taaluma ya sheria
kwa kutoa huduma bora kwa umma.
Post a Comment