Serikali yamsimamisha Kazi Mtendaji Mkuu wa DART, Bi ASTERIA MLAMBO
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wanahabari
nimewaita hapa leo ili mnisaidie kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu mradi
wetu wa Mabasi yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam (DART – BRT).
Kama
mnavyofahamu Serikali ilianzisha mradi huu ili kupunguza msongamano wa magari
barabarani kwa madhumuni ya kurahisisha usafiri na usafirishaji katika Jiji
letu.
Kutokana na kukamilika
kwa sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza ya mradi, Serikali
iliamua tuwe na mtoa huduma wa mpito (Interim Service Provider) kabla ya
kumpata mtoa huduma wa kudumu (Service Provider).
Mtoa huduma wa mpito alipaswa
kupatikana kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hata hivyo, Serikali
imebaini ukiukwaji wa wazi wa sheria hiyo wakati wa kumpata mtoa huduma wa
kipindi cha mpito.
Kufuatia hali hiyo
nimeamua kumsimamisha kazi kuanzia leo tarehe 23 Desemba, 2015, Mtendaji Mkuu
wa DART, Bi. Asteria Mlambo ili kupisha uchunguzi.
Bi Asteria Mlambo |
Sababu za
kumsimamisha kazi ni:
i.
Kushindwa kuzingatia Sheria ya
Manunuzi ya Umma wakati wa kumpata mtoa huduma katika kipindi cha mpito;
ii.
Kushindwa kuchukua hatua hata pale
alipobaini kuwa mtoa huduma wa mpito amekiuka masharti ya mkataba wa kutoa
huduma ya mpito;
iii.
Kufanya maamuzi makubwa pasipo
kuishirikisha Bodi ya Ushauri ya DART.
Aidha, Serikali
inatambua kuwa wapo watumishi wa DART ambao hawakumshauri vizuri Mtendaji Mkuu.
Watumishi hao watachunguzwa na kuchukuliwa hatua na Kaimu Mtendaji Mkuu
atakayeteuliwa.
Nimemwagiza Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelea na taratibu za kinidhamu dhidi ya
Mtendaji Mkuu aliyesimamishwa kazi.
Naitumia nafasi
hii kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa haraka na
uangalifu ili mradi huu uweze kuanza kutoa huduma bora ya usafiri kwa wakazi wa
Dar es salaam bila kuchelewa zaidi.
Aidha, natoa rai kwa wananchi kuitunza na kuithamini miundombinu ya DART
kwa kuwa imegharimu fedha nyingi kwa manufaa yao.
Imetolewa
na:-
George B.
Simbachawene,
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mheshimiwa George Simbachawene akizungumza na
Wanahabari kuhusu kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa DART, Bi. Estaria Mlambo
kuanzia leo tarehe 23.
|
Post a Comment