Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha
na Maalim Seif Sharif Hamad ,Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amekutana naMakamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Mgombea Urais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharrif Hamad, leo tarehe 21
Desemba, 2015 Ikulu Jijini Dar es Salaam
kufuatia maombi yake ya siku nyingi.
Mazungumzo ya Viongozi hao pia yamehudhuriwa na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Viongozi hawa kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar na
wamefurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea. Aidha, Mhe. Rais
Magufuli amewapongeza Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim
Seif Sharif Hamad, na viongozi wote wanaoshiriki katika mazungumzo ya kuleta
hali ya uelewano Zanzibar.
Rais Magufuli pia amewapongeza
na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu wakati wa
mazungumzo baina ya viongozi wa CUF na CCM yakiendelea huko Zanzibar.
Katika Mazungumzo hayo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif
Sharrif Hamad amemueleza Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania juu ya hali ya siasa Zanzibar kadiri anavyoielewa yeye
na Rais Magufuli amemshukuru Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa
taarifa yake nzuri huku akimsihi waendelee na mazungumzo hadi suluhisho muafaka
lipatikane.
Majadiliano yanayoendelea yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na
sifa njema ya nchi yetu. Wote kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa
watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema.
Wameelezea matumaini yao kuwa vyama vya CCM na CUF haviwezi kushindwa kupata
suluhu ya mgogoro huo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemuhakikishia kuwa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano itahakikisha kuwa amani na utulivu unaendelea kudumishwa
Zanzibar.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
21Desemba, 2015
|
Post a Comment