Serikali yatahadharisha Makampuni ya Simu
(Picha na Hassan Silayo)
WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
TAARIFA
KWA UMMA KUHUSU KANUNI MPYA ZA HUDUMA ZA ZIADA ZA MWAKA 2015 ZA SHERIA YA
MAWASILIANO YA KIELEKTRONIKI NA POSTA YA MWAKA 2010
(THE
ELECTRONIC AND POSTAL COMMUNICATION ACT 2010 (VALUE ADDED SERVICES) REGULATIONS
2015)
Ndugu Waandishi wa Habari
1.
Awali ya yote namshukuru
Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutupatia uhai na afya njema na kutuwezesha
kukutana leo kupeana taarifa kuhusu Kanuni Mpya za Huduma za Ziada za Mwaka
2015 ambazo zinatokana na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya
Mwaka 2010. Napenda pia kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kukubali mwito kushiriki
nasi katika siku hii ya leo. Karibuni sana.
Ndugu waandishi wa Habari
2. Sekta
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) imeendelea kukua kwa kasi
duniani na hapa nchini kwetu na imeleta mafanikio mengi katika nyanja
mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwenye ngazi ya kitaifa na kwa
mwananchi mmoja mmoja katika maisha ya kila siku kwa waishio mijini na vijijini.
Idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini imeendelea kuongezeka kutoka
line za simu za viganjani milioni 2.96 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 32.1
mwezi Desemba 2014. Watumiaji wa mfumo wa intaneti nao wameongezeka kutoka
milioni 3.56 mwaka 2008 hadi kufikia milioni 11.34 mwaka 2014. Mafanikio haya yanathibitika nanyi mmekuwa ni
mashahidi kwa kuongezeka kwa huduma za mawasiliano na huduma za ziada za
matumizi ya mitandao ambapo imerahisisha kutoa na kupata huduma kwa haraka na
kwa wakati; na wananchi hawalazimiki
kusafiri; na kupunguza urasimu kama vile huduma za kutuma na kupokea pesa;
kulipia ankara za maji, umeme, ada; ukusanyaji wa mapato; kulipia leseni;
kusafirisha taarifa na data; huduma mtandao kama vile Serikali mtandao,
biashara mtandao, shule mtandao na tiba mtandao. Kwa mfano kuna ongezeko kubwa
la huduma za ziada kupitia mawasiliano ya simu za kiganjani. Huduma hizo ni
pamoja na miamala ya kifedha ambayo ina watumiaji wapatao 12,330,962 na ununuzi
wa huduma na bidhaa kwa kutumia miamala ya kibenki. Hivi sasa, wananchi
wanaweza kufanya malipo ya huduma mbalimbali wanazozitumia kupitia simu za
kiganjani ambapo katika kipindi cha Julai, mwaka 2013 hadi Aprili, mwaka 2014
jumla ya miamala 972,641,605 yenye thamani inayofikia shilingi Trilioni 28.3
imefanyika. Maendeleo haya yamesaidia kuokoa muda na kupunguza msongamano
sehemu za kulipia na kupata huduma hizi.
3.
Aidha, mafanikio hayo
yameleta changamoto mbalimbali kwenye Sekta na katika jamii yetu. Kwa leo
tunazungumzia uwepo wa changamoto ya utoaji wa huduma za ziada kwa watumiaji wa
huduma za ziada bila kuwa na utaratibu unaoeleweka kati ya mtoa huduma na mpokea
huduma au mlaji. Baada ya kujitokeza kwa
changamoto katika utoaji wa huduma za ziada, Serikali kupitia Wizara ya
Mawasiliano Sayansi na Teknolojia ilitunga Kanuni Mpya za Huduma za Ziada za
Mwaka 2015 (Value Added Services - VAS Regulation 2015). Kanuni hizo
zimetangazwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe 7 Mwezi Agosti mwaka huu 2015
na kupewa GN. Namba. 320. Kanuni hizo zimetokana na Sheria ya Mawasiliano ya
kielektroniki na Posta ya Mwaka 2010 (The Electronic and Postal Communication
Act 2010) iliyotungwa na kuridhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
mnamo tarehe 29 Januari 2010 na badae kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 20
Machi 2010.
Ndugu Wananchi
4.
Lengo kuu la Kanuni
za VAS ni kuweka utaratibu mahususi unaoleweka wa utoaji na upokeaji wa huduma za ziada.
Huduma za ziada ni huduma za mawasiliano za kielektroniki zinazotolewa kupitia
mitandao zaidi ya huduma za msingi za mawasiliano. Kanuni za VAS zimeweka
utaratibu kwa mlaji kujiunga na kujiondoa kupata huduma za ziada; wajibu wa
mtoa huduma na mlaji wa huduma za ziada; pamoja na adhabu pindi matakwa ya kanuni
yatakapokiukwa. Kimsingi kanuni hizi humlinda mlaji wa huduma za mawasiliano
asipewe huduma ambazo hajaridhia kupitia huduma za ziada zinazotolewa na watoa
huduma za mawasiliano.
Ndugu Waandishi wa Habari
5.
Kanuni za VAS zinamtaka
mtoa huduma za ziada kutoa taarifa kamili na sahihi kuhusu huduma za ziada
katika lugha rahisi na ya uwazi. Lugha zinazotakiwa kutumika kwa mujibu wa
Kanuni zetu Mpya ni Kiswahili na Kiingereza tu. Mtoa huduma za ziada atakuwa na
wajibu ufuatao katika kutoa huduma kwa mlaji;
i.
Kutoa masharti na
vigezo vya huduma zote ikiwemo gharama, kwa njia ya kielektroniki na kudurufu
(printed and electronic formats);
ii.
Ikiwa mhusika
mwingine atahusishwa katika utoaji wa huduma hiyo (third party), mlaji anapaswa
kujulishwa kuhusu hitaji ama utegemezi wa huduma hizo kutoka kwa mhusika
mwingine;
iii.
Kuzingatia matakwa ya
Kanuni za Viwango vya Huduma (Quality of Service - QoS) za Sheria ya EPOCA;
iv.
Ikiwa kutakuwepo na
mabadiliko katika huduma, mlaji apatiwe
taarifa kamili kuhusu masharti ya uhamaji, ikiwa ni pamoja na mabadiliko katika
utoaji wa huduma hizo na gharama endapo zitajitokeza;
v.
Kumjulisha mlaji juu
ya waranti za bidhaa zilizotolewa kwa ajili ya kutumika pamoja na huduma ikiwa
ni pamoja na jinsi ya kupata waranti hizo.
Ndugu
waandishi wa habari
6.
Kanuni zinamtaka mtoa
huduma za ziada, kuweka mfumo wa kuwezesha huduma za ziada kwa mlaji kujiunga (opt
in / activation) au kujiondoa (opt out/de-activation) ambao ni rahisi na wa
uwazi kwa kutumia teknolojia inayofaa ikiwemo ujumbe wa meseji (SMS), Huduma ya
sauti (Interactive Voice Request – IVR), namba maalum (Unstructured
Supplementary Service Data – USSD) ama mchanganyiko wa teknolojia hizi.Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania itawajibika katika kutoa namba (short code) kwa watoa
huduma za ziada ili kuwezesha huduma hizo kupitia teknolojia zilizotajwa.
7.
Mlaji anaweza
kujiunga (opt in/activation) ili kupatiwa huduma za ziada kwa njia tajwa hapo
juu. Ili kujiunga kwa njia ya SMS, mtoa huduma za ziada atatoa taarifa ya uwepo
wa huduma za ziada kupitia menyu ya huduma, meseji wakati wa maulizo ya salio,
ama meseji ya uthibitisho wa kuongeza salio. Ili kusajili huduma ya ziada
katika namba yake, mlaji atachagua kutoka katika menyu ya huduma au kutuma
ujumbe mfupi wenye chaguo la huduma anayoihitaji.
Mlaji atapokea ujumbe kutoka
kwa mtoa huduma za ziada ikieleza masharti na vigezo vya huduma hiyo, ikiwemo
gharama za huduma; kipindi ambacho huduma imewezeshwa; na namna ya kujiondoa
katika huduma hiyo. Baada ya kuridhika na masharti na vigezo, mlaji
atathibitisha ili huduma hiyo kuwezeshwa katika namba yake. Baada ya hapo, mtoa
huduma za ziada atatuma ujumbe wa kuthibitisha kuwezeshwa kwa huduma iliyoombwa
(activation).
8.
Aidha, kwa kutumia njia
ya sauti (IVR) na namba maalum (USSD), pindi mlaji atakapopiga namba ya IVR ama
USSD, mlaji atapokea tangazo lililorekodiwa ama orodha ya huduma za ziada
zinazopatikana pamoja na masharti na vigezo ikiwa ni pamoja na gharama na
kipindi cha huduma hizo. Baada ya mlaji kuchagua kwa kubonyeza kitufe
kinachohusika, atapokea uthibitisho ndani ya dakika 15 kwamba maombi ya
kuwezeshwa kwa huduma yamepokelewa na yanashughulikiwa. Mlaji atapokea tangazo
lililorekodiwa kwamba huduma iliyochaguliwa imewezeshwa. Ikiwa amekosea
kubonyeza kitufe, mlaji atataarifiwa na orodha kurudiwa tena.
9.
Kanuni zinamtaka mtoa
huduma za ziada, kuweka mfumo wa kumuwezesha mlaji kujiondoa katika huduma za
ziada (opt out/de-activation) ambao ni rahisi na wa uwazi kwa kutumia ujumbe wa
maandishi (SMS) ama Huduma ya sauti (Interactive Voice Request – IVR). Mamlaka
inawajibika kutoa namba (short code) kwa watoa huduma za ziada ili kuwezesha
mlaji kujiondoa katika huduma hizo.
10.
Ili kumuwezesha mlaji
kujiondoa kwenye huduma za ziada kwa kutumia njia ya SMS, mlaji atatuma ujumbe
mfupi wa maandishi; au kutumia njia ya sauti kwa kupiga namba ya IVR au USSD
ambapo mlaji atapokea ujumbe unaomjulisha orodha ya huduma za ziada
zilizowezeshwa katika namba yake na kuchagua huduma anayohitaji ili iweze kuondolewa.
Mtoa huduma atatuma ujumbe wa maandishi unaohitaji mlaji athibitishe nia yake
ya kutaka kujiondoa katika huduma husika. Baada ya kupokea uthibitisho wa
kujiondoa kutoka kwa mlaji, mtoa huduma za ziada ataondoa huduma hiyo katika
namba ya mlaji. Endapo ikitokea mlaji amekosea, mtoa huduma za ziada atatuma
ujumbe mfupi wa maandishi ili kumjulisha mlaji kuhusu kosa lililopo na chaguo
la kurudia zoezi husika. Baaada ya mlaji kufanikisha kujiondoa, mtoa huduma za
ziada atatuma ujumbe kuthibitisha kwamba huduma iliyochaguliwa imeondolewa
katika namba ya mlaji.
11.
Aidha, Ili mlaji
aweze kujiondoa katika huduma za ziada kwa njia ya sauti (IVR), baada ya kupiga
namba ya IVR, mlaji atapata tangazo lililorekodiwa lenye orodha ya huduma za
VAS zilizowezeshwa katika namba yake.
Baada ya kukubaliana na masharti na vigezo, mlaji atachagua huduma ya
ziada ya kuondolewa kwa kubonyeza kitufe kinachohusika na atapokea uthibitisho
ndani ya sekunde sitini kwamba ombi la kujiondoa limepokewa na linafanyiwa
kazi. Iwapo atakuwa amebonyeza kitufe kisichohusika, mlaji atajulishwa na
orodha ya huduma za ziada itarudiwa ili zoezi hilo liweze kurudiwa. Ikiwa mlaji
atakosea kwa mara nyingine simu yake itahamishiwa katika kituo cha huduma kwa
mteja (call centre) cha mtoa huduma za ziada.
Ndugu waandishi wa
habari
12.
Katika kutoa
matangazo ya promosheni ya huduma za ziada, mtoa huduma za ziada atazingatia
Kanuni za Sheria ya EPOCA za kumlinda mteja (Consumer Protection) za mwaka
2011. Mtoa huduma atatangaza kwa mlaji aidha wakati wa kuuliza salio, ama
kupitia meseji ya uthibitisho baada ya kuongeza salio ama katika menyu ya mtoa
huduma.
Mtoa
huduma za ziada hatajihusisha katika kutoa matangazo yasiyoombwa na mlaji kwa
njia ya kielektroniki ila tu pale ambapo aidha mlaji ameridhia, ama mwanzoni
mwa mawasiliano ataweka wazi utambulisho wa mtoa huduma za ziada (ama mhusika
aliyepo kwa niaba) na madhumuni ya mawasiliano hayo; ama mawasiliano yanatoa
mchanganuo wa gharama za bidhaa ama huduma ambayo inahusika katika mawasiliano.
Ndugu wananchi
13.
Kwa mujibu wa Kanuni
Mpya za Huduma za Ziada za Mwaka 2015, Mlaji anawajibu ufuatao;
i.
Kuridhia huduma kwa
kukubali masharti na vigezo vya huduma kama ilivyoelekezwa katika kanuni hizi;
ii.
Baada ya kuridhia
masharti na vigezo vya huduma kutoka kwa mtoa huduma za VAS, mtumiaji atabanwa
na masharti na vigezo hivyo.
14.
Aidha, ni vema ieleweke
kuwa kwenye Kanuni ya kumi (10) ya
Kanuni hizi Mpya za Huduma za Ziada Kanuni hiyo inaelekeza kuwa mtu yoyote
atakayekiuka vipengele vya Kanuni hizi anatenda kosa kisheria na atawajibika
kulipa faini ambayo si chini ya shilingi milioni tano ama kifungo kisichozidi
miezi mitatu ama vyote kwa pamoja. Kanuni Mpya inapatikana kwenye tovuti ya
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia www.mst.go.tz
15.
Natoa rai kwa watoa
huduma za ziada kuwa waendelee kuzingatia Kanuni hizi katika kuwapatia wateja
wao huduma za ziada zenye bora na viwango vinavyotakiwa na walaji kuhakikisha
kuwa wanapatiwa huduma za ziada inayostahili na waliyoomba kwa kuwa teknolojia
imerahisha utaratibu wa utoaji na upokeaji wa huduma za ziada.
Imetolewa
na;
Prisca
J. Ulomi
Msemaji
Wizara
ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia
Asanteni kwa kunisikiliza.
Post a Comment