Kesi Rufaa ya Talaka Dhidi ya MTEMBEI yaahirishwa
Na Mwandishi wetu
KESI ya rufaa ya madai ya talaka dhidi ya mfanyabiashara na Mkurugenzi wa shule ya sekondari ya St Mathew, Thadei Mtembei imeahirishwa baada ya wakili wa Mtembei, Mussa Kyoboya kudai mrufaniwa yuko India kwa matibabu.
Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Tarimo.
Katika kesi hiyo, mpeleka rufaa, Magreth Mwangu anawakilishwa na wakili Chacha Mrungu. Kesi hiyo ilikuja mahakamani juzi ambapo mrufaniwa alitakiwa kupeleka majibu ya rufaa.
Hata hivyo, wakili wake alisema majibu hayako tayari kwani kuna vipengele ambavyo alitakiwa kusaini, lakini ilishindikana kutokana na kuwa nchini India kwa matibabu. Kesi hiyo imepangwa kuendelea Desemba 16 mwaka huu.
Awali, kesi hiyo ilisikilizwa katika Mahakama ya Mwanzo Kizuiani mbele ya hakimu Rajab Tamaambele, ambapo Mwangu na watoto wake walionekana hawana haki, kwa madai sio mke halali na watoto hao ni wa zinaa kutokana na kuzaliwa nje ya ndoa.
Katika madai ya msingi, Mwangu anataka talaka, mgawanyo wa mali na matunzo ya watoto.
Katika sababu za rufaa, mrufani alieleza kusikitishwa na maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Mwanzo Kizuiani Septemba Mosi mwaka huu, kwa hakimu kukosea kisheria kwa kutosaini nakala ya hukumu ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa saini za wazee wa baraza.
Sababu nyingine ni Mahakama kukosea kisheria kwa kunyang’anya haki ya watoto kwa kutotoa matunzo ya watoto kwa mama, ambaye anaishi na mrufaniwa kwa miaka 20 na kuvunja Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009. Maamuzi ya Mahakama ya Kizuiani yalishindwa kufuata sheria kwa wazee wa baraza kushindwa kutoa maoni yao.
Post a Comment