Header Ads

Mamlaka ya Bandari TANZANIA yatakiwa Kupunguza Idadi ya Vikao Visivyo na Tija

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kupunguza idadi ya vikao vya baraza visivyo na ulazima ili kuondokana na matumizi mabaya ya fedha na badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye uendelezaji wa miundombinu ya  bandari za maziwa.

Ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua shughuli za utendaji  wa bandari ya Kasanga iliyopo mkoani Rukwa inayohudumia mkoa wa Kigoma, nchi ya Burundi na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC)  ambapo amebaini mapungufu ya kiutendaji ikiwemo malipo yasiyotumia njia za kielektroniki na miundombinu isiyo rafiki katika kukidhi ushindani wa kibiashara katika bandari hiyo.

Waziri Mbarawa ameitaka TPA kuweka mfumo wa uendeshaji vikao kwa njia ya kieletroniki (video conference) kwa lengo la kudhibiti matumizi ya fedha nyingi zilizokuwa zikitumika katika uendeshaji wa vikao hivyo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Rukwa Arch. Deocles Alphonce wakati alipokagua ujenzi  wa ofisi za  Bonde la Ziwa Rukwa na Maabara zake zilizopo Sumbawanga Mjini.

“Nataka TPA muanze kutumia video Conference katika vikao vyenu ili fedha zilizokuwa zikitumika zifanyie kazi nyingine za maendeleo ya Taifa”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Ameongeza kuwa TPA  imekuwa na wajibu mkubwa wa kuchangia pato la Taifa kupitia huduma za upakiaji na upakuaji wa mizigo hivyo wanapaswa kuanza kutumia mfumo wa kielekroniki katika ukusanyaji wa mapato katika bandari zote nchini ili kudhibiti upotevu wa mapato.

“Tukianzisha mfumo wa kielekroniki katika bandari hii tutakuwa na uwezo wa kufuatilia mapato yanayopatikana katika utoaji wa huduma na kujua kama malengo yamefikiwa”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua nondo zilizosukwa kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Kalambo lililopo katika barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga yenye urefu wa KM 112, Mkoani Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akihakiki taarifa za mapato katika Bandari ya Kasanga iliyopo Mkoani Rukwa, Katikati ni Msimamizi wa bandari hiyo Bw. Seleman Kalugendo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa Maelekezo kwa Meneja wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL)  nyanda za juu kusini Bw. Peter Kaguru wakati alipotembelea ofisi hizo Mkoani Rukwa.

No comments

Powered by Blogger.