Header Ads

Serikali yasisitiza Umuhimu wa Utunzaji Nyaraka kwa Waombaji Kazi


Msemaji wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bi. Riziki Abraham (kushoto) akiongea na waandishi wa Habari kuhusu Umuhimu wa Utunzaji Nyaraka kwa waombaji kazi katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Jijini Dar es Salaam, kulia ni Naibu katibu anayehusika na Udhibiti na Ubora Bw. Humphrey Mniachi.
Naibu Katibu Kutoka Sekretarieti ya Ajira anayesimamia Idara ya Udhibiti na Ubora Bw. Humphrey Mniachi  akitoa Ufafanuzi wakati wa Mkutano na Waandishi wa habari kuelezea Umuhimu wa Utunzaji Nyaraka kwa waombaji kazi kushoto ni Msemaji wa Sekretarieti ya Ajira Bi. Riziki Abraham.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Bi. Riziki Abraham (Kushoto) akionyesha vipeperushi kwa waandishi wa Habari vinavyoelezea utekelezaji wa Mchakato wa Ajira Serikalini kulia ni Naibu katibu Ofisi hiyo anayehusika na Udhibiti na Ubora Bw. Humphrey Mniachi.
Sehemu ya  waandishi wa habari wakifuatilia Mkutano huo.
(Picha na Fatma Salum)

Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma katika kutekeleza jukumu lake la uendeshaji wa mchakato wa Ajira serikalini imekuwa ikikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya matukio ya upotevu wa vyeti vya kitaaluma na nyaraka nyingine za msingi kutoka kwa waombaji kazi.
Tunaendelea kusisitiza na kuwakumbusha wadau wetu  kwamba miongoni vya vigezo vya msingi vinavyotumiwa na Sekretarieti ya Ajira pamoja na Waajiri ili kujua kama muhusika anayeomba kazi ana sifa na vigezo vinavyotakiwa katika nafasi husika ni pamoja na kuwa na vyeti vya kuhitimu taaluma husika.
Takribani waombaji kazi 256,928 wamekosa fursa ya kuitwa kwenye usaili ili kuweza kuajiriwa Serikalini kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kutokuwa na vyeti vya kitaaluma, kutozingatia vigezo vya tangazo la kazi, kuomba nafasi ya kazi ambayo mwombaji hana sifa zinazokidhi nafasi hiyo.
Kumekuwa na tatizo kutoka kwa baadhi ya Waombaji kazi wengi kutotambua umuhimu wa kutunza Vyeti vyao vya kitaaluma na nyaraka nyinginezo kama vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa, hati ya kusafiria pamoja na barua za utambulisho.
Imekuwa ni kawaida kwa waombaji kazi wanaowasilisha maombi ya ajira kukuta baadhi yao hawana vyeti kwa maelezo kuwa vyeti/cheti kimepotea/kimeibiwa, kimeungua, kimeliwa na panya, kiliingia maji ya mafuriko na baadhi yao kutunziwa vyeti na wazazi wao kama ''Custodian'' wao wa kuhifadhi vyeti ama nyaraka husika.
Baada ya kukutana na changamoto hizi, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma itaendelea kuimarisha mifumo yake ya utambuzi ili waombaji kazi wasio na vigezo wasiweze kupata fursa ya kuajiriwa katika Utumishi wa Umma. Hii inatokana na sababu kwamba kuwaajiri watu wasio na sifa katika Utumishi wa Umma kuna athari kubwa katika maendeleo ya Nchi yetu na ina athari kwa jamii yote ya Watanzania.
Sekretarieti ya Ajira inapenda kuwasisitizia wadau wake  hususani waombaji kazi kuwa ni muhimu wakatambua vyeti ni ajira, vyeti ni maisha, vyeti ni utambulisho na uthibitisho.

 Kwa kuwa hakuna anaeweza kuajiriwa serikalini bila ya kuwa na vyeti halisi na halali maana Serikali inaendesha mchakato wa Ajira kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu na si vinginevyo. 

Hivyo ni vyema wakavihifadhi katika sehemu iliyo salama ili kuvitumia pindi vinapohitajika na kwa wale waliopoteza, kuibiwa, kuungua wakatoe taarifa kwa mamlaka husika ili waweze kujua taratibu za kufuata ili kuweza kuendelea kupata huduma katika mamlaka mbalimbali.

Aidha, chombo hiki kitaendelea kukagua nyaraka zinazowasilishwa  na waombaji kazi ili kubaini wale wote wasiokuwa na sifa stahili pamoja na wanaotumia vyeti vya kughushi kwa ajili ya kupata kazi serikalini ili kuhakikisha kuwa watu wa namna hiyo hawapati nafasi ya kuingia katika Utumishi wa Umma.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma. 23 Desemba, 2015.


No comments

Powered by Blogger.