Waziri Mkuu KASSIM MAJALIWA apokea Taarifa ya Mgogoro wa Loliondo
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea Taarifa ya Kamati Shirikishi ya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo ya kushughulikia mgogoro wa matumizi ya
ardhi kwenye pori tengefu la Loliondo mkoani Arusha, ambapo atatoa maelekezo
baada ya kuisoma.
Amepokea taarifa hiyo leo (Alhamisi,
Aprili 20, 2017) katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Spika, Bungeni
mjini Dodoma, Aliiunda Kamati hiyo, Desemba
mwaka jana, mara baada ya kumaliza ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Kiini cha mgogoro huo ni eneo la pori tengefu la Loliondo ambalo
linagombewa na wawekezaji, wakulima, wawindaji kwa sababu ni mapitio ya
wanyama, chanzo cha maji, mazalia ya wanyama, malisho ya mifugo na makazi.
Waziri Mkuu amesema lengo la kamati
hiyo ni kutaka kupata muafaka wa matumizi ya rasilimali zilizoko katika eneo
hilo ili kila upande uweze kutekeleza majukumu yake bila ya kuathiri mwingine
na kuwezesha wananchi wote kunufaika na rasilimali zilizoko katika eneo hilo.
“Serikali inataka watu
wote tuwe kitu kimoja katika kutunza maeneo yetu, lakini pia shughuli za
wananchi nazo ziweze kuendelea ili Watanzania wote tuweze kunufaika na rasilimali
zilizoko kwenye maeneo yetu,” amesema.
Waziri Mkuu amesema
Serikali inapenda kuona maeneo yote nchini yakiwa katika hali ya utulivu bila ya kuwepo kwa migogoro ya aina yoyote na
ikitokea ni vema ikawa inapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili shughuli za maendeleo
ziweze kufanyika kwa ufasaha.
Post a Comment