Serikali yaendelea Kutoa Elimu Juu ya Madhara ya Ndoa za Utotoni
Serikali imeendelea kuchukua hatua kwa kuendelea kutoa elimu katika Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Miji 72 ili kuondokana na tatizo la ndoa za utotoni zinazobababisha watoto kukosa haki ya msingi ya kupata elimu.
Akijibu swali la Mhe. Anna Kilango Malecela Mbunge wa Viti Maalum (CCM) lililouliza Je, Serikali ina Mkakati gani wa kutokomeza ndoa za utotoni? Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsi Wazee na Watoto Mhe. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa msisitizo utazidi kuwekwa katika utoaji wa elimu kwa familia, wazee wa mila na jamii kwa ujumla.
“Tutajikita kutoa elimu zaidi ili jamii iachane na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati za kuoza watoto wa kike” alisisitiza Mhe. Dkt. Kigwangalla.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua athari kubwa zinazosababishwa na ndoa za utotoni katika jamii ya watanzania na itaongeza nguvu katika kutoa elimu na kupambana na wale wote watakaojihusisha kwa namna moja au nyingine kuwanyima watoto wa kike haki yao ya kupata elimu.
Aidha kulingana na takwimu za Afya na Idadi ya Watu nchini za mwaka 2016 ndoa za utotoni zimeshamiri katika mikoa ya Shinyanga kwa asilimia 59, Tabora kwa asilimia 58, Mara kwa asilimia 55 na Dodoma kwa asilimia 51 hivyo Serikali itaendelea kupambana kutokomeza ndoa za utotoni nchini.
Kwa upande wa muundo wa kisera na kisheria, Serikali imezifanyia maboresho Sera na Sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa na mimba za utotoni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Elimu Sura 353 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yoyote atakayempa mimba mwananfunzi wa shule ya Msingi au Sekondari.
Katika kutokomeza ndoa na mimba za utotoni Serikali itaanza utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto mwezi June 2017 unaojumuisha Sekta zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo la kutokomeza aina zote za ukatili na kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi 10 ifikapo mwaka 2020.
Post a Comment