Header Ads

Bodi ya Maziwa Tanzania Kushirikiana na Sekta Binafsi Kuongeza Idadi ya Ng'ombe wa Maziwa

Bodi ya Maziwa Tanzania imeandaa Mpango Mkakati  wa ushirikiano na Sekta Binafsi ili kuongeza idadi ya ng’ombe wa maziwa kufikia Milioni 1.5 hatua inayolenga kuongeza wa soko la uzalishaji wa mazao ya maziwa katika nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa Nchini, Nelson Kilongozi wakati wa mahojiano katika kipindi maalum cha TUNATEKELEZA kinachorushwa hewani na Shirika la Utangazaji Nchini (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO).

Kilongozi alisema taasisi hiyo imeandaa mkakati huo wa miaka 5 kuanzia mwaka 2018-23 ili kuhakikisha kuwa viwanda vya Tanzania vinakuwa na uwezo mkubwa wa kusindika maziwa na kushindana na nchi nyingine za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya katika uuzaji na usambazaji wa mazao ya maziwa katika ukanda wa Jumuiya hiyo.

“Kwa sasa Tanzania ina jumla ya Ng’ombe wa maziwa 782,000 kati ya ng’ombe Milioni 28 waliopo, hivyo hawatoshelezi mahitaji yetu, lengo letu ni kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa tasnia ya maziwa inaleta tija inayokusudiwa” alisema Kilongozi.

Kwa mujibu wa Kilongozi alisema uzalishaji wa maziwa nchini kwa sasa ni lita Bilioni 2.1 kwa mwaka ambapo asilimia 70 yanatokana na ng’ombe wa asili, ambapo hata hivyo imekuwa ni vigumu kutoa elimu kwa wafugaji wake kutokana na changamoto ya kuhama mara kwa mara kwa ajili ya kutafuta malisho.

 Aliongeza kuwa kuwa mpaka sasa kuna jumla ya viwanda 82 vyenye uwezo wa kusindika lita laki 652,000, na hivyo Bodi hivyo imejipanga katika kuhakikisha kuwa inaongeza hamasa kwa wawekezaji kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo na vya kati ili kulinda ubora wa maziwa ya Tanzania.

“Changamoto iliyopo sasa ni kukosekana kwa vituo vya ukusanyaji wa maziwa pindi yanapozalishwa kwa kuwa vituo hivyo havina vifaa vya kupoozea maziwa pindi yanazalishwa kabla ya kufikishwa kiwandani” alisema Kilongozi.

Alisema Bodi hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa wafugaji kuzingatia kanuni za ufugaji bora ikiwemo kuwa na mbegu bora zenye uwezo wa kuzalisha kiasi kikubwa cha cha maziwa ili waweze kujiongezea kipato sambamba na kuimarisha afya.

Akifafanua zaidi Kilongozi alisema Bodi hiyo pia imeendelea kuhamasisha wananchi kujenga tabia ya kunywa maziwa kwa, ambapo kwa mwaka huu wataanzisha Programu maalum ya uhamasishaji unywaji wa maziwa katika mikoa 6 nchini.


Aliitaja Mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Iringa, Njombe na Mbeya, ambapo pamoja na mambo mengine program hiyo imelenga pia kukabiliana na magonjwa ya udumavu yanayowakabili watoto wadogo katika mikoa mbalimbali nchini.

No comments

Powered by Blogger.