Serikali yadhamiria Kuwekeza Kwenye Vifaa tiba Vitokanavyo na Pamba
Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unakamilisha taratibu za uwekeza kwenye vifaa tiba vitokanavyo na pamba na bidhaa za maji ya dripu(Infusion Fluids).
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge mjini Dodoma.
“Gharama za miradi hii inakadiriwa kufikia dola za kimarekani milioni 36.5 na kutoa ajira za moja kwa moja 1600 na zisizo za moja kwa moja 5000”, Alisema Mhe.Mwijage.
Amesema mradi huu unakadiriwa kutumia pamba tani elfu 50 kwa mwaka na Serikali ya Mkoa wa Simiyu inaendelea na jitihada za kutenga maeneo ya uwekezaji kwa kuwalenga wajasiriamali wadogo,wa kati mpaka wakubwa bila kujali kama ni wa kutoka ndani au nje ya nchi.
Aidha amesema kuwa azma ya Serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda imeainishwa vyema katika mpango wa pili wa Maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016/17-2020/21 wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Pamoja na hayo ameainisha kuwa ili kufikia azma hiyo ushiriki wa mchango wa mtu mmoja mmoja,makundi ya watu,taasisi za umma na taasisi binafsi unahitajika.
Amebainisha mikakati minne ambayo imeanza kufanyiwa utekelezaji ni ya ngozi,mafuta ya kula,nguo na mazao jamii ya kunde uku wakati huohuo mpango wa wilaya moja,zao moja na uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda chini ya SIDO unaendelea nchini kote.
Post a Comment