Dkt. Mwakyembe awa mgeni rasmi Tamasha la Michezo la Wanawake
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe (Mb) ameshiriki na kuwa mgeni rasmi katika kilele cha
Tamasha la Michezo la Wanawake lililoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa
(BMT).
Tamasha hilo limefanyika mapema leo 8 Aprili, 2017 katika
Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Felix Lyaniva, pia washiriki
mbalimbali toka kwenye Wizara, Taasisi za Serikali, binafsi pamoja na wanafunzi
kutoka shule za msingi na sekondari.
Akihutubia hadhira iliyokuwepo uwanjani hapo, Dkt. Mwakyembe
amewahamasisha wanawake kushiriki kikamilifu kwenye mazoezi mara kwa mara ili
kulinda afya zao ikiwemo kuibua vipaji vya wasichana wadogo ambao ndiyo mbegu
ya mafanikio katika sekta ya michezo.
“Serikali itaendelea kuipatia michezo kipaumbele kwa
kuboresha Sera zote zinazogusa masuala ya michezo na elimu ya mazoezi ya
viungo, kutenga bajeti ya kutosha kutoka katika ngazi zote kuanzia shuleni,
vijijini, kata, Halmashauri/Wilaya, Mikoa, kutoa mafunzo mbalimbali pamoja na
uhamasishaji wa ushiriki wa wananchi katika michezo”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi wote nchini kuachana na mila
na tamaduni ambazo zinazuia wanawake kushiriki kwenye michezo.
Post a Comment