Health Nusu Marathon Kufanyika Dar Aprili 26
Taasisi ya Tanzania Health Summit yaandaa mbio za
nusu Marathon na Upimaji wa afya kwa lengo la kusaidia juhudi za serikali katika
kupunguza magonjwa yasioambukiza, mbio hizo zinazotarajia kufanyika Aprili 26
katika barabara ya Kaole iliyopo Masaki jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo
Rebecca John wakati alipokutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa
lengo la kuhamasisha jamii kushiriki.
“Kamati ya maandalizi ya ya mbio za Heart Marathon inapenda
kuwa taarifu wadau wote wa sekta ya afya hapa nchini na jamii kwa ujumla juu ya
mbio za Heart Marathon na upimaji wa afya ili kuungana na serikali katika
juhudi za kupunguza magonjwa yasiyoambukiza” alisema Rebecca.
Aliongeza kuwa kwa mwaka huu mbio hizi
zitashirikisha washiriki zaidi ya elfu mbili kutoka rika mbalimbali wakiwemo
vijana, watoto, wazee, makundi ya watu wenye ulemavu na watu wenye magonjwa
yasiyoambukiza.
Pia washiriki watapata nafasi ya kupima afya
magonjwa mbalimbali kama vile shinikizo la damu ,wingi wa sukari katika damu, kiasi
cha mafuta mwilini, uchunguzi wa uvimbe katika matiti na kupata ushauri wa
wataalam kuhusiana na vyakula bora, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Aidha Bi. Rebecca aliongeza kuwa washiriki
watakimbia umbali tofauti, kwani kuna mbio ndefu za kilometa 21.1 kwa ajili ya
wakimbiaji wazoefu, kilometa 10 kwa wakimbiaji wa kati, kilometa 5 kwa
wakimbiaji wa kawaida, kifamilia na kampuni na mbio za watoto chini ya miaka 12
ni meta 700 na zawadi itatolewa kwa mshindi wa kilometa 21.1 pekee kwa kiasi
cha shilingi laki tano.
Kwa upande wake Rais wa Tanzania Health Summit
Dr.Omary Chillo alisema kuwa washiriki watatakiwa kutoa kiasi kidogo cha fedha
kwa ajili ya kununua flana pamoja na
kifaaa maalum cha kuhesabia muda wakati wa kukimbia ila maji ya kutosha yatatolewa
bure kwa ajili ya wakimbiaji.
Aliongeza kuwa wameimarisha ulinzi kwa kushirikiana
na jeshi la polisi na ili kulinda usalama kwa washiriki na wananchi
watakaokuwepo katika mashindano hayo.
“wananchi wasiwe na wasiwasi wa usalama kwani
tutashirikiana na jeshi la polisi ili kuimarisha usalama na tumeweza kupata baraka
nyingi kutoka kwao kwa kuweza kushirikiana nao” aliongeza Chillo.
Pia Katibu msaidizi wa Chama cha Riadha nchini Bi
Ombeni Zavala alisema anashukuru wananchi wanavyoweza kujitokeza katika
mashindano hayo na pia anawaomba wananchi hasa vijana waendelee kujitokeza kwa wingi kwani wanaweza
kupata nafasi ya kuunda timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17.
Naye Sajenti Isaya Mlokozi kutoka kanda ya usalama
barabarani alisema jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani litahusika
vizuri katika sehem inayowahusu kuhakikisha watu wanafanya zoezi hilo kwa hali
ya usalama na litajumuika na wananchi popote pale watakapokuwa wanakwenda.
Mashindano haya mwaka jana yalifanyika katika Chuo
Kikuu Cha Dar es Salaam lakini kutokana na kuongezeka kwa watu mwaka huu
yatafanyikia barabara ya kaole yenye kauli mbiu ‘piga hatua moja mbele ya
magonjwa sugu’
Post a Comment