Header Ads

Jeshi la Polisi Nchini Latangaza Kiama Kwa Majambazi Nchini


Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, CP. Nsato Marijani Mssanzya akizungumza na wa  Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu Operesheni Maalum iliyoanzishwa na Jeshi hilo kufuatia tukio la Askari wake 8 kuuwawa na Kundi la Majambazi katika eneo la  Mkengeni, Wilayani Kibiti, Pwani jana. Kushoto ni Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Advera Senso.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano baina yao na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Tanzania, CP. Nsato Marijani Mssanzya kuhusu tukio la Askari wake 8 kuuwawa na Kundi la Majambazi katika eneo la  Mkengeni, Wilayani Kibiti, Pwani jana.

.................................

Na: Frank Shija – MAELEZO

Jeshi la Polisi Nchini limetangaza Operesheni Maalum itakayokuwa muarubaini wa kudhibiti matukio ya ujambazi ambayo yameanza kujirudia hapa nchini ili kuhakikisha raia wa Tanzania pamoja na mali zao wanabaki salama.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi CP. Nsato Marijani Mssanzya wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam kuhusu hatua zilizochukliwa na Jeshi hilo kufuatia tukio la kuuwawa kwa askari 8 lililotokea jana katika maeneo ya Mkengeni, Wilayani Kibiti, Pwana.

Kamishna Marijani alisema kuwa Jeshi la Polisi limepokea kwa amsikitiko makubwa taarifa ya uhalifu huu ambapo tayari wamekwisha anza Operesheni Maaalum itakayo hakikisha wahusika wote wanachukuliwa hauta stahiki.

“Niseme tu kuwa sasa umefika mwisho hatuwezi kuvumilia uhalifu wa namna hii uendelee kushamiri nchini kwetu, sisi kama Jeshi lenye dhamana ya kulinda raia na mali zao tuko imara, tutawashughulikia kikamilifu wahalifu wote, dawa ya moto ni moto, haiwezekani Askari wetu takribani 10 sasa wapoteze maisha kisha tunyamaze, tumeanza Operesheni Maalum itakayofanyika nchi nzima kwa lengo la kuhakikisha tunamaliza mtandao wa uhalifu hapa nchi,” alisema Kamishna Marijani.

Kamishna Marijani aliongeza kuwa baada ya tukio la jana, Jeshi la Polisi lilichukua hatua za Kiintelijensia na Upelelezi zilizopelekea kubaini maficho ya muda ya majambazi hao ambapo Askari walifanikiwa kuwadhibiti na kufanikiwa kuuwa majambazi wanne na kupata bunduki nne  ambazo mbili kati yake zilikuwa nizile zilizoporwa na majambazi hao katika tukio la jana.

Katika hatua nyingine Kamishna Marijani ametangaza kuwa kuanzia sasa waendesha Pikipiki wote wa maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji Mkoani Pwani, hawataruhusiwa kufanya shughuli za bodaboda baada ya saa 12:00 jioni.

Awali akisoma taarifa hiyo, Kamishna Marijani aliwataja Askari Polisi walipoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Peter Kigugu, F.3451 Koplo Francis,F.6990 PC Haruna,G.3247 PC Jackson, H.1872 PC Zacharia,H.5503 PC Siwale,H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub.


Tukio la kuvamiwa na kuuwawa kwa Askari hao lilitokea jana tarehe 13/04/2017 majira ya 12:15 jioni katika maeneo ya Mkengeni,Kata ya Mjawa, Wilayani Kibiti Mkoani Pwani, ambapo kundi la majambazi ambao idadi yao haijafahamika wakiwa na silaha za moto walishambulia kwa risasi gari la Polisi lenye namba PT.3713 Toyota Land Cruiser lililokuwa limebeba Askari 9 ambapo mmoja kati yao alijeruhiwa sehemu ya mkono na tayari ameshapatiwa matibabu na kuruhusiwa.

No comments

Powered by Blogger.