Header Ads

Pence: Marekani Haitaivumilia tena Korea Kaskazini

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence amesema kipindi cha taifa hilo kuwa na subira na Korea Kaskazini kimepita.
Bw Pence alisema hayo alipozuru eneo ambalo haliruhusiwi kuwa na wanajeshi katika mpaka wa Korea Kaskazini na Korea Kusini.
Ziara yake imetokea kipindi ambacho hali ya wasiwasi imeendelea kutanda katika rasi ya Korea, huku Marekani na Korea Kaskazini zikijibizana vikali.
Bw Pence aliwasili mjini Seoul Jumapili saa chache baada ya Korea Kaskazini kutekeleza jaribio la kurusha kombora, ambalo halikufanikiwa.
Jumatatu, Marekani na Korea Kusini zilianzisha mazoezi ya pamoja ya majeshi yake ya wanahewa, kuhakikisha kwamba wanajeshi wake wako tayari kwa tishio lolote kutoka kwa Korea Kaskazini, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Korea Kusini.
Bw Pence, ambaye babake alipigana katika Vita vya Korea, alikuwa akihutubu katika kijiji cha Panmunjom siku ya Jumatatu.



 Ni katika kijiji hicho ambapo mkataba wa kumaliza vita vya Korea ulitiwa saini.
Aliwaambia wanahabari: "Kumekuwepo na kipindi cha subira, lakini kipindi hicho cha subira kimemalizika."
Marekani inataka kuhakikisha kuna usalama katika rasi hiyo ya Korea "kupitia amani, kupitia mashauriano," alisema.
Lakini "njia nyingine zozote" zinaweza kutumiwa.
Aliyasema hayo muda mfupi baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson kusema Marekani inaweza kuishambulia Korea Kaskazini (kuzuia mashambulio ya Korea Kaskazini) alipozuru eneo hilo lisiloruhusiwa kuwa na wanajeshi mwezi uliopita.Bw Pence pia alikariri kujitolea kwa Marekani kuisaidia Korea Kusini na akasema ni ushirikiano thabiti.
Aliitahadharisha Korea Kaskazini na kusema haifai kuwa na shaka kuhusu kujitolea kwa Marekani kuwatetea washriika wake.
Aidha, alishutumu jaribio la karibuni la makombora la Korea Kaskazini na kusema ni "uchokozi".
Jumatatu, Bw Pence pia alizuru Camp Bonifas, ambayo ni kambi ya kijeshi ya Umoja wa Mataifa karibu na eneo lisiloruhusiwa wanajeshi mpakani.
bw Pence anazuru Korea Kusini, Japan, Indonesia na Australia kwenye ziara hiyo yake ya siku 10 katika bara la Asia.

No comments

Powered by Blogger.