Bomba Kubwa la Kusambazia Maji Lafika Jijini Dar es Salaam
Mafundi wakiendelea na kazi ya kulaza mabomba ya Maji eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam. Mabomba hayo ambayo sasa yamekamilika kwa urefu wa kilometa 54.8 kati ya 55.9 yatatumika kusafirisha maji kutoka mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini, Bagamoyo mkoani Pwani.
Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA,
Romanus Mwang’ingo (katikati) akitoa ufafanuzi kuhusu maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa bomba hilo la kusafirishia Maji kutoka Ruvu Chini kuelekea
matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha Ardhi ambao umefika eneo la Mbezi Beach
jijini Dar es salaam.
Maneja wa Kampuni ya Gauff Consultants, Thorsten Seitz akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari kuhusu maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa bomba hilo la kusafirishia Maji kutoka Ruvu Chini.
Na. Aron Msigwa - Dar es salaam
Huduma ya Usambazaji wa Maji Safi katika jiji la
Dar es salaam inatarajiwa kuimarika kwa kuwafikia wananchi wengi zaidi mwishoni
mwa mwezi Februari mwaka huu kufuatia kukamilika kwa kilometa 54.8 za mradi wa Ujenzi
wa Bomba kubwa la kusambazia Maji kutoka chanzo cha Maji cha Ruvu Chini.
Mradi huo unajengwa na Kampuni ya JBG Gauff
Ingenieure kwa gharama ya shilingi Bilioni 141 ambazo zimetolewa na Serikali ya
Tanzania una jumla ya urefu wa kilometa 55.9.
Akizungumzia mradi huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi
wa Usimamizi na Ufundi wa DAWASA, Romanus Mwang’ingo amesema kuwa mpaka sasa
ujenzi wa bomba hilo kuelekea matangi ya kuhifadhia maji ya Chuo Kikuu cha
Ardhi umefika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam na huku ikiwa imebakiza kilometa
1.1.
Amesema ujenzi
wa mradi huo kutoka mtambo wa Ruvu Chini ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la
maji katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani na kuongeza kuwa
utakapokamilika utazalisha lita milioni 270 kwa siku kutoka lita milioni 182 ambazo
zote zitasukumwa kuja jijini Dar es salaam.
Aidha,
amesema kasi ya mkandarasi ya kulaza bomba hilo inaridhisha licha ya kuwepo kwa
changamoto mbalimbali zinazochelewesha kazi hiyo zikiwemo za ufinyu wa eneo
linapojengwa bomba hilo kuwezesha mitambo kufanya kazi vizuri katika eneo la
mbezi Beach, mvua zinazoendelea kunyesha ,changamoto ya makazi ya watu kuwa
ndani ya mradi ambapo kulikuwa na kesi 17 Mahakamani zikihusisha madai
mbalimbali ya wananchi katika maeneo hayo.
“Ni kweli zipo changamoto zilizosababisha mradi
kukawia kumalizika zikiwemo za wananchi kufungua kesi 17 Mahakama ya Ardhi, hadi sasa DAWASA tumeshinda
kesi 14 ndiyo maana tumepata haki ya
kutumia njia hii kukamilisha upanuzi wa mradi” Amesema Mwang’ingo.
Ameongeza kuwa lengo la mradi huu nikuongeza
uzalishaji wa maji na kuboresha huduma kwa wakazi wa maeneo ya uwekezaji (EPZ)
Bagamoyo, Chasimba, Buma, Zinga, Kerege na Mpiji mkoa wa Pwani.
Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huo kwa
Mkoa wa Dar es Salaam ni Bunju, Wazo, Salasala, Madale na Kinzudi Mbezi Juu,
Goba, Kawe, Makongo, Mwenge, Msasani, Mikocheni, Mlalakua, Masaki, Sinza,
Kijitonyama, Manzese, Konondoni, Magomeni, Kigogo na Vingunguti.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Kampuni inajenga
bomba hilo nchini Muhandisi Eric Omuruli akizungumzia mradi huo amesema kuwa
yeye kama Meneja mradi atahakikisha anashughulikia changamoto zilizopo ili
kukamilisha kwa wakati.
Amesema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto
mbalimbali katika eneo la mradi hasa eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam
kampuni ya JBG Gauff Ingenieure inafanya kila linalowezekana ili mradi huo
ukamilike mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.
“Tumejipanga kufanya kazi hadi usiku kupunguza
muda,kazi iliyobaki ni ndogo, tunawahakikishia DAWASA tutaimaliza kazi hii
mwishoni mwa mwezi huu” Amesisitiza.
Post a Comment