Header Ads

DAWASCO yanasa Nyumba Tano kwa Wizi wa Maji eneo la Tabata Jijini Dar es Salaam

Fundi wa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (Dawasco), akiondoa bomba la maji lililounganishwa kinyume cha taratibu katika moja ya nyumba iliyopo eneo la Tabata Magengeni jijini Dar es Salaam. Dawasco imeanza operesheni wizi wa Maji iliyoanza hivi karibuni katika maeneo yote ya jiji la Dar es salaam. 

Na Mwandishi wetu

Shirika la Majisafi na Majitaka Jijini Dar es Salaam (Dawasco), imenasa wizi mkubwa wa Maji katika nyumba tano ambazo zimeunganishiwa huduma ya majisafi kinyume cha utaratibu maeneo ya Tabata Magengeni, nyumba hizo zinamilikiwa na mfanyabiashara mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, nyumba hizo zimepangishwa kwa familia tano tofauti (Apartments).


Akizungumzia tukio hilo katika operesheni ya mtaa kwa mtaa ya kuhakiki matumizi sahihi ya Maji kwa wateja wa majumbani, Meneja wa Dawasco Tabata, Bi. Victoria Masele, alisema kuwa amebaini wizi huo baada ya kuona bili ya mwezi inayokuja haiendani na matumizi halisi ya Maji, hivyo wakaamua kufanya uchunguzi na kubaini kuwa mteja alikuwa amejiunganishia huduma ya Maji kinyume cha taratibu.


Msoma mita wetu alikuwa na wasiwasi sana na matumizi ya Maji ya hizi nyumba, kwa sababu bili ilikuwa ndogo ukilinganisha na idadi ya familia zinazoishi kwenye hizi nyumba, ndipo tukaamua kufanya uchunguzi wa kina na kukuta mteja amejiunganishia laini 3 za Maji, laini 1 ikiwa imepita kwenye mita, 2 hazijapita kwenye mita, zimeelekezwa kwenye kisima na baadaye Maji yanasukumwa na kujaza matenki 5 ya lita 10,000, na lingine la lita 6000”


Baada kunasa wizi huo, tuliwasiliana na meneja wa nyumba hizo ambaye hakuwepo eneo la tukio, na kudai kuwa hajui chochote kuhusiana na wizi huo wa Maji kutokana na kuishi mbali na nyumba hizo na kwamba wizi huo inawezekana wa wapangaji wenyewe, lakini aliahidi kufika katika ofisi zetu za Dawasco kumaliza tatizo baada ya wapangaji kushindwa kutupa ushirikiano” alisema Bi. Masele


Hadi taarifa hizi zinakwenda mtamboni, meneja wa nyumba hizo alifika katika ofisi za Dawasco Tabata na kufanya mazungumzo na Meneja wa kituo, na kutakiwa kulipa faini ya kiasi cha shilingi milioni 5.3.


DAWASCO inaendelea kutoa rai kwa wananchi wote kuwafichua wezi wa Maji kwa kuwa wanasababisha wateja halali kukosa huduma ya Maji kwa wachache kujiunganishia huduma kinyume na taratibu, hivyo mwananchi yeyote ambaye amejiunganishia Maji kinyume cha taratibu na ambaye hana huduma ya Maji afike katika ofisi yoyote ya Dawasco iliyopo karibu yake ili aunganishiwe huduma ya Maji kihalali.

No comments

Powered by Blogger.