Wizara ya Afya yaagiza Kufungwa kwa Chumba cha Upasuaji Hospitali ya SANITAS iliyoko Mikocheni Jijini Dar es Salaam
Naibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla ameagiza kufungwa mara moja Chumba cha upasuaji cha hospitali ya Sanitas ya Mikocheni Jijini Dar es Salaam baada ya kubaini kuwa na kasoro mbalimbali ikiwemo mfumo na ramani yake kimefungwa kwa kutokidhi vigezo vya kimataifa vya namna chumba hicho kinavyotakiwa kuwa.
Dk. Kigwangalla ametoa agizo hilo mapema jana Februari 29.2016, alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye hospitali hiyo majira ya saa nane na nusu mchana ambapo baada ya kutembelea hospitali nzima na kushuhudia namna ya utolewaji wa huduma, hakuridhishwa na hali aliyokutana nayo kwenye chumba hicho na kutoa maagizo kwa Msajili wa Hospitali Binafsi, Dkt. Pamela Sawa kufunga chumba hicho mpaka uongozi wa hospitali hiyo utakapofanya marekebisho ya mapungufu yaliyopo.
“Chumba cha upasuaji hakiko sawa, siwezi kuvumilia kuacha chumba hiki kiko chini ya kiwango cha kimataifa. Rekebisheni chumba hiki kwa kutumia mfumo wa ramani wa wizara,” alieleza Dkt. Kigwangalla wakati wa kutoa maagizo kwa mmoja wa Ofisa wa Hospitali hiyo.
Aidha uongozi wa hospitali hiyo umepewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo ya kutowalipa mishahara kwa kipindi cha miezi minne watumishi wake pamoja na jinsi wanavyoteketeza taka hatarishi za hospitali hiyo.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo alipata malalamiko kutoka kwa watumishi hao ambao wamelalamikia kukatwa kwa makato ya mafao pasipo kupelekwa mahali husika kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu.
Dkt. Kigwangalla alivitaja viwango vya chumba cha upasuaji kuwa kinatakiwa chumba cha kubadilishia mavazi,kunawa mikono,sehemu ya alama maalum zenye rangi nyekundu, meza ya upasuaji, ukanda wa usafi, chumba cha mapunziko baada ya kutoka kwenye upasuaji na chumba cha kusafishia vifaa vya upasuaji na kuna mashine maalum kwa kuwa kila upasuaji una idadi ya vifaa vinavyotumika.
Aliongeza kuwa viwango hivi vinawekwa ili kuepuka maambukizi.
Kwa upande wake Meneja Uendeshaji wa hospitali hiyo, Bi. Gean Cabral alisema watarekebisha mapungufu yaliyobainika pamoja na kufanya yale yote waliyoagiziwa baada ya tukio hilo.
Tazamatukio hilo hapa:
Imeandaliwa na Magreth Kinabo, (MAELEZO).
Naibu wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamisi Kigwangalla (katikati) akipata maelezo machache kutoka kwa Meneja uendeshaji wa Hospitali ya Sanitas, Bi. Gean Cabral wakati walipowasilia katika ziara hiyo..
Dk Kigwangalla akikagua baaadhi ya sehemu katika hospitali hiyo.
Dk. Kigwangalla akizungumza na baadhi ya wagonjwa (hawapo pichani) namna Serikali ya Rais Magufuli inavyofanya kazi kwa kusimamia haki na usawa ikiwemo kufika katika maeneo yenye kero na kuchukua hatua ilikumuokoa Mwananchi katika kupata haki yake na huduma bora anayostahiki.
Dk. Kigwangalla akitoa maagizo hayo kwa Meneja uendeshaji wa hospitali hiyo, Bi. Gean Cabral.
Dk. Kigwangalla akimuonesha moja ya 'karatasi' iliyoandikwa ujumbe mbalimbali dhidi ya madai kutoka kwa wafanyakazi wa Hospitali hiyo.
Meneja Uendeshaji wa Hospitali hiyo Bi. Gean Cabral akifafanua jambo pamoja na Naibu Waziri wakati wa ziara hiyo..
Dk Kigwangalla akiangalia namna hali ya Maabara ya Hospitali hiyo licha ya kuwa na vifaa vya kutosha, lakini imeshindwa kuweka mpangilio mzuri unaotakiwa kutumika katika maabara. ikiwemo suala la usafi.
Naibu Waziriwa Afya, Dk. Kigwangalla (kushoto), Msajili wa Hospitali Binafsi pamoja na maafisa wengine akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dk. Aziz (kulia) wakijadiliana jambo muda mfupi baada ya kumalizika kwa ziara hiyo ya kushtukiza kuangalia namna ya uendeshaji katika huduma za Sekta za Afya, zikiwemo za Serikali na zile za watu binafsi. (Picha zote na Andrew Chale).
Post a Comment