Hali ya Unyonyeshaji Nchini sio Nzuri
Imeelezwa kuwa wastani wa unyonyeshaji kwa watoto walio chini ya miezi sita nchini sio mzuri na hivyo kuwa na uwezekano wa watoto kudhoofika kwa kukosa maziwa ya mama ambayo yanakuwa na virutibisho muhimu kwa ukuaji ya mtoto.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dkt. Joyceline Kaganda katika warsha iliyoandaliwa na UNICEF ili kujadili jinsi uwekezaji mkubwa zaidi katika kunyonyesha maziwa ya mama kunaweza kusaidia maendeleo kiuchumi na kuokoa maisha ya watoto nchini.
Dkt. Kaganda amesema wastani wa unyonyeshaji kwa watoto walio chini ya miezi sita ni asilimia 42 na wastani huo ni mdogo hivyo kuashiria kuwa hali sio njema kwa watoto ambao hawapati maziwa ya mama.
Amesema kiafya inatakiwa mtoto aanze kunyonya nusu saa baada ya kuzaliwa na mtoto anyonye maziwa ya mama yake kwa kipindi kisichopungua miezi sita na baada ya hapo anaweza kuanza kuwa anachanganya na vyakula vingine kama uji na maji.
“Hali sio nzuri ukiangalia wastani wa wamama ambao wanawapa watoto wao maziwa ya kunyonya ni wachache na labda inawezekana wengi wakawa hawatambui matatizo yanayoweza kutokea kama hawatawanyonyesha watoto wao,” amesema Dkt. Kaganda.
Aidha Dkt. Kaganda amesema kazi zinachangia kina mama wengi kushindwa kuwanyonyesha watoto wao lakini wanaweza kuweka utaratibu wa kuwa wanakamua maziwa yao na kuyahifadhi sehemu nzuri ili hata kama wanapokuwa mbali na watoto wao, msimamizi anayemuangalia mtoto aweze kumpa mtoto ili kumfanya apate virutubisho muhimu kutoka kwenye maziwa ya mama yake.
Nae Mwakilisha wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Bi. Maniza Zaman amesema katika kusaidia Tanzania kuongeza wastani wa watoto ambao wananyonya wamekuwa wakitoa elimu kwa kina mama wanaonyonyesha pamoja na familia zao ili wajue umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa ya mama.
Alisema watoto wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa matatizo ambayo yanatokana na kukosa maziwa ya mama zao na hivyo ili kuzidi kushughulikia tatizo hilo wanataraji kuanza kutoa elimu kwa watumishi wa afya katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe na wanataraji kutembelea zaidi maeneo ya vijijini kutokana maeneo hayo kuonekana kutokuwa na elimu hiyo zaidi.
“Watoto wamekuwa wakipata matatizo na kupoteza maisha na hiyo inachangiwa na kutokunyonya kwa mama … tumeshirikiana na serikali tunataraji kutoa elimu katika vijiji zaidi ya 15,000 kwenye mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya na tutafundisha pia mama na familia umuhimu wa mtoto kunyonya,” alisema Bi. Zaman.
Alisema baada ya kumalizika kwa mikoa hiyo wataendeleza utoaji wa elimu nchi nzima ili jamii ya Tanzania itambue umuhimu wa watoto kunyonya maziwa ya mama na pia kuwaomba waandishi wa habari kutumia nafasi yao katika jamii ili kuwaelimisha watanzania kuhusu tatizo hilo.
Katika makala zilizoandikwa katika jarida la habari za afya la The Lancet linaonyesha kuwa uboreshaji wa kunyonyesha maziwa ya mama kunaweza kuokoa maisha zaidi ya watoto 820,000 kila mwaka duniani na Dola za Kimarekani Bilioni 302 kila mwaka.
Imendaliwa na Rabi Hume
Mwakilisha wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Bi. Maniza Zaman akitoa neno la ufunguzi katika warsha iliyoandaliwa na UNICEF ili kujadili jinsi uwekezaji mkubwa zaidi katika kunyonyesha maziwa ya mama kunaweza kusaidia maendeleo kiuchumi na kuokoa maisha ya watoto nchini.(Picha zote na Rabi Hume)
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dkt. Joyceline Kaganda katika warsha iliyoandaliwa na UNICEF akielezea hali ya unyonyeshaji kwa watoto ilivyo nchini.
Baadhi ya wadau wa sekta ya afya waliohudhuria katia warsha hiyo wakifatilia kwa makini ripoti zilizokuwa zikitolewa.
Mshauri Mwandamizi wa maswala ya watoto wadogo na unyonyeshaji kutoka Makao Makuu ya UNICEF, New York, Dr. France Begin akielezea kuhusu makala za The Lancet juu ya uwekezaji mkubwa zaidi katika kunyonyesha maziwa ya mama jinsi kunavyoweza kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kuokoa maisha ya watoto nchini.
Mshauri Mwandamizi wa maswala ya watoto wadogo na unyonyeshaji kutoka Makao Makuu ya UNICEF, New York, Dr. France Begin akiwaonyesha wahudhuriaji wa warsha hiyo ripoti ya utafiti uliofanywa na jarida la The Lancet linalohusika na kuandika habari za afya.
Viongozi wa Taasisi mbalimbali waliofika katika warsha hiyo wakifatilia ripoti ya utafiti uliofanywa na jarida la The Lancet. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Lishe katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Dkt. Vicent Assey, Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu,Obey Assery Nkya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dkt. Joyceline Kaganda na Mwakilisha wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Bi. Maniza Zaman.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Obey Assery Nkya akielezea hatua ambazo serikali imechukua ili kupunguza idadi ya kina mama ambao hawanyonyeshi watoto.
Viongozi wa Taasisi mbalimbali waliofika katika warsha hiyo wakisikiliza maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wadau wa sekta ya afya na waandishi wa habari. Wa kwanza kulia ni Mshauri Mwandamizi wa maswala ya watoto wadogo na unyonyeshaji kutoka Makao Makuu ya UNICEF, New York, Dr. France Begin, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Lishe katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Dkt. Vicent Assey, Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Shughuli za Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu,Obey Assery Nkya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe, Dkt. Joyceline Kaganda na Mwakilisha wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Bi. Maniza Zaman.
Mkuu wa kitengo cha fedha na malipo nchini kutoka Benki ya Dunia, Douglas Pearce akiuliza swali katika warsha hiyo.
Mwakilisha wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini, Bi. Maniza Zaman akitoa neno la shukrani kuashiria kumalizika kwa warsha hiyo.
Post a Comment