Header Ads

Serikali yawataka Mawaziri Kurejesha Fomu za Maadili Kabla ya Saa 12 Jioni Leo

kas1
Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi ya Waziri Mkuu wakati alipotoa maagizo ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kuhusu mawaziri ambao bado hawajajaza fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni wawe wamejaza fomu hizo na kuzirejesha katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam ifikapo leo saa 12.00 jioni (Ijumaa, Februari 26, 2016).

kas2
Waziri Mkuu Mh. Majaliwa Kassim Majaliwa akiendelea kufafanua mambo kadhaa kwa wanahabari katika mkutano huo kushoto ni WAZIRI wa nchi,ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala bora, Mh Angella Kairuki.
.......................................................

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amesema mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni wawe wamejaza fomu hizo na kuzirejesha katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam ifikapo leo saa 12.00 jioni (Ijumaa, Februari 26, 2016).

Agizo hilo la Rais limetolewa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mbele ya waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es Salaam.

“Mheshimiwa Rais ameelekeza mawaziri ambao hawajajaza tamko la rasilmali au hati ya ahadi ya uadilifu wafanye hivyo na kuzirejesha kabla saa 12 jioni na Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema wakati akifungua mafunzo ya Mawaziri na Naibu Waziri kuhusu Mwongozo wa Maadili ya Viongozi wa Umma na Utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu yaliyofanyika Ikulu jana (Alhamisi, Februari 25, 2016) alikabidhiwa majina ya Mawaziri na Naibu Mawaziri ambao hawajawasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili.

Amewataja mawaziri wanaotakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi (OMR – Muungano na Mazingira), Bw. January Makamba.

 Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga ambaye anatakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako ambaye anatakiwa kutoa tamko la rasilmali na madeni.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira), Bw. Luhaga Mpina anatakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilmali na madeni pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.

No comments

Powered by Blogger.