Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu TANZANIA ( TIA ) chafanyika Mkoani Mororgoro
Na Mwandishi wetu,
Morogoro.
WITO umetolewa kwa
watumishi wa Umma kufanya kazi kwa uadilifu na kutimiza wajibu wao kikamilifu
katika sehemu zao za kazi.
Wito huo umetolewa na
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji wakati akifungua kikao
cha tatu cha Baraza kuu la Pili la Wafanyakazi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania
(TIA), katika ukumbi wa TAFORI mkoani Morogoro.
Dkt. Kijaji amesema
kuwa, Serikali haitamvumilia mtumishi wa ngazi yeyote wa wizara ya Fedha na
Mipango atakayeshindwa kutimiza wajibu wake kikamilifu ikiwa ni pamoja na
kushindwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Naibu Waziri huyo
ameuagiza uongozi wa Taasisi hiyo kuendelea kusimamia kwa karibu kazi zote na
kutathimini utendaji kazi wa watumishi wake.
“Haipendezi kukuta meza
ya Mkurugenzi imejaa majalada huku watumishi wa chini yake wakiwa hawana kazi
za kufanya” alisema Naibu Waziri huyo.
Dkt. Kijaji amesisitiza
kuwa, wakati umefika kwa kuwapatia watumishi hao kazi za kufanya ili nao wapate
uzoefu ambao tayari viongozi waliopo ngazi za juu wameshaupata.
Pamoja na mambo
mengine, Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango amewataka watumishi wa Serikali
wakiwemo wa Wizara hiyo kila mmoja wao kuwajibika katika nafasi yake
kwani suala hilo ni muhimu katika kuleta tija sehemu ya kazi.
“Sasa ni wakati wa
watumishi wa umma kujituma pamoja na kufanyakazi kwa bidii kwa kuwa
mmepewa dhamana ya kuwatumikia watanzania wote “ amesema Naibu Waziri huyo.
Nae Afisa
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Dkt. Joseph Kihanda,
amesema kuwa Taasisi imejiimarisha katika utoaji wa elimu yenye ubora ili
kuwawezesha wahitimu kufanya vizuri katika masomo yao na baadaye katika sehemu
zao za kazi.
Amesema jitihada zao za
kutoa elimu bora zimethibitishwa na bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi
(NBAA) na bodi ya Wataalamu wa manunuzi na ugavi (PSPTB).
Hata hivyo Afisa
Mtendaji Mkuu huyo amesema Taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto
mbalimbali zinazoikabili kwa muda mrefu ikiwemo ya uhaba wa majengo kwani kwa
kipindi cha miaka minane Taasisi hiyo imekuwa ikiomba ruzuku Serikalini
kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini bado haijapata ruzuku hiyo.
Pia ameitaja
changamoto nyingine kuwa ni pamoja na uhaba wa wafanyakazi ambapo uwiano
wa wahadhiri haulingani na wanafunzi.
Hali hiyo inatokana na
Taasisi kupata vibali vichache vya kuajiri wahadhiri na wafanyakazi waendeshaji
kutoka Utumishi ikilinganishwa na maombi ya Taasisi.
Post a Comment