Rais Dkt MAGUFULI aagiza Mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha NYANZA Zirudishwe
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuchunguza na kuchukua hatua za kurejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika
cha Nyanza ambazo zilinunuliwa na
kutwaliwa na watu binafsi kwa njia za ujanja ujanja.
Rais Magufuli
ametoa agizo hilo leo tarehe 11 Agosti, 2016 alipokuwa akiwahutubia wananchi wa
Mwanza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha Jijini
Mwanza.
Dkt. Magufuli
amesema Serikali yake haipo tayari kuwafumbia macho watu wachache waliovifilisi
vyama vya ushirika vya wakulima kwa kujimilikisha mali za ushirika yakiwemo
majengo, viwanda na mashamba na ametaka mali hizo zirudishwe mikononi mwa
wananchi.
"Hata kama
walichukua miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue hatua na mali hizo zirudishwe
kwa umma" Amesema Rais Magufuli.
Katika Mkutano huo
Rais Magufuli pia amesema Serikali itafanya oparesheni kubwa ya kuteketeza Makokoro
katika ziwa Victoria ikiwa ni juhudi za kukabiliana na tatizo la uvuvi haramu
uliosababisha kupungua kwa samaki na kuathiri shughuli za uvuvi na usindikaji
wa minofu ya samaki katika viwanda.
Amebainisha kuwa
lengo la kuchukua hatua hiyo ni kuwezesha samaki wengi kuzaliana ili lengo la
Serikali la kujenga viwanda vya kusindika mazao ikiwemo viwanda vya kusindika
minofu ya samaki lifanikiwe.
Kabla ya kuhutubia
mkutano huo Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la waenda
kwa miguu la Furahisha linalokatiza barabara ya Uwanja wa Ndege kwenda katikati
ya Jiji la Mwanza.
Daraja hilo
litakuwa na urefu wa meta 46, upana wa meta 3.6 na kimo cha meta 5.5 na ujenzi
wake unatarajiwa kukamilika Mwezi Desemba Mwaka huu kwa gharama ya Shilingi Bilioni
6.455.
Akizungumzia
ujenzi huo Rais Magufuli amemtaka Mkandarasi anayejenga Daraja la Furahisha
kukamilisha kazi hiyo Mwezi Desemba Mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, na pia
ameagiza Mkandarasi aliyekuwa akifanya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kuendelea
na kazi hiyo ndani ya wiki moja kwa kuwa Serikali imejipanga kumlipa fedha za
kazi hiyo.
Pia Dkt. Magufuli
ameahidi kuongeza fedha katika ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Katikati
ya Jiji la Mwanza hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza ili barabara hiyo ifike hadi
uwanjani badala ya kuishia eneo la Pasiansi.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza
11 Agosti,
2016
Post a Comment