Header Ads

Naibu Waziri wa Nishati aagiza Malipo ya Fidia Mradi wa Umeme SOMANGA FUNGU


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya Maendeleo ya TIB kuhakikisha kuwa kuanzia Agosti 17 mwaka huu, wanaendelea kuwalipa fidia wananchi watakaopitiwa na mradi wa usafirishaji umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Somanga Fungu  wilayani Kilwa hadi Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri alitoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao chake na Wawakilishi wa wananchi watakaopitiwa na mradi huo, Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Benki ya Maendeleo ya TIB.

Kikao hicho kilichofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini kililenga katika kuweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa fidia hiyo pamoja na kuunda Kamati itakayofuatilia utekelezaji wa malipo kwa wananchi watakaopitiwa na mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO. Hii ni baada ya kuonekana kuwa ulipaji wa malipo hayo ulikuwa ukisuasua na hivyo wananchi kuilalamikia Serikali.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kulia) akisalimiana na Wawakilishi wa Wananchi watakaopitiwa na mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Somanga Fungu hadi jijini Dar es Salaam utakaotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO, Wawakilishi hao walifika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini ili kujadili ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo,  Kikao hicho pia kilihudhuriwa na watendaji kutoka TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini na  Benki ya Maendeleo ya TIB.

Naibu Waziri alisema kuwa jumla ya fedha inayopaswa kulipwa kwa wananchi hao katika wilaya za Temeke, Mkuranga, Kilwa,  Ilala na Kinondoni ni shilingi bilioni 79 na kwamba mpaka sasa Serikali imeshalipa shilingi bilioni 32.7 na kiasi kilichobaki ni shilingi 46.3.

Hivyo katika kiasi hicho kilichobaki cha shilingi bilioni 46.3, Naibu Waziri aliziagiza TANESCO  na TIB kupunguza deni hilo kwa kuanza kuwalipa shilingi bilioni 7.3, Wananchi wa Kivule na Rufiji ambao watapitiwa na mradi  huo ambapo fedha zitaanza kutolewa kuanzia tarehe 17 mwezi huu na ukomo wake ni tarehe 22 Septemba mwaka huu.

" Hivyo nimewaelekeza TANESCO na TIB kuanza kulipa malipo hayo Tarehe 17 mwezi huu ambapo wataanza kulipa shilingi bilioni 1. 9, hilo ndio elekezo la kwanza na awamu ya kwanza," alisema Dkt. Kalemani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kulia) akiwa katika kikao na Wawakilishi wa Wananchi watakaopitiwa na mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 kutoka Somanga Fungu hadi jijini Dar es Salaam utakaotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO. 

Alisema kuwa malipo mengine yatafanyika  tarehe 27 mwezi huu ambapo Taasisi hizo zitalipa shilingi bilioni 1.03 kwa wananchi, tarehe 8 mwezi wa 9 mwaka huu Taasisi hizo zitalipa shilingi  bilioni 1.60 na tarehe 15 mwezi wa Tisa zitalipa shilingi  bilioni 1.53 ambapo malipo ya mwisho kufanyika  ni tarehe 22 Septemba mwaka huu pale ambapo Taasisi hizo zitalipa shilingi bilioni 1.2  na hivyo watu wa Kivule na Rufiji watakuwa wamekamilika.

Dkt Kalemani aliongeza kuwa baada ya Awamu ya Kwanza ya malipo kukamilika mwezi Septemba mwaka huu,  malipo hayo ya fidia yataendelea kufanyika katika sehemu nyingine zenye madai hayo huku lengo likiwa ni kumaliza madai husika  mwezi Oktoba mwaka huu.

Kuhusu uundaji wa Kamati ya kufuatilia malipo hayo ya fidia, Dkt. Kalemani alipendekeza Mwenyekiti wa Kamati hiyo atoke upande wa wananchi watakaopitiwa na mradi huo ili kufuatilia kwa karibu malipo hayo kwa wananchi, ambapo pendekezo hilo liliridhiwa na Wawakilishi  wa wananchi pamoja na Watendaji wa Serikali.

Katika kikao hicho, Wawakilishi hao wa wananchi walimchagua Ndugu Josephat Haule kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo huku Katibu wa Kamati akitoka Wizara ya Nishati na Madini. Wajumbe wa Kamati hiyo wanatoka upande wa Wananchi, TANESCO, TIB na Wizara ya Nishati na Madini.

Aidha, Naibu Waziri alitoa angalizo kuwa, mwananchi yeyote atakayewasilisha madai ya uongo au kuweka majina hewa ili alipwe fidia  atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha kwa nyakati tofauti Wawakilishi hao wa wananchi walimpongeza Naibu Waziri kwa kuamua kulivalia njuga suala hilo  ili kuwezesha mradi huo kutekelezeka kwa ufanisi na kuhakikisha wananchi wanapata haki yao.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia umeme, Mhandisi Innocent Luoga, alisema kuwa,  kukamilika kwa ulipaji wa fidia kwa wananchi hao kutawezesha kuanza kwa ujenzi wa njia hiyo ya kusafirisha umeme wa  msongo wa kV 400.

Alisema kuwa umeme utakaosafirishwa  na miundombinu hiyo utatoka katika mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia itakayojengwa na kampuni ya Kilwa Energy katika eneo la Somanga wilayani Kilwa ambapo mitambo hiyo  itazalisha umeme wa kiasi cha megawati 320.

Vilevile alisema kuwa Serikali ilichukua jukumu la kulipa fidia hiyo kwa wananchi mwaka 2015, hivyo  baada ya tathmini kukamilika,  fedha hizo zimeanza kulipwa na Serikali mwaka huu  kupitia Benki ya Maendeleo ya TIB.


No comments

Powered by Blogger.