( MAKALA ) Tuunge Mkono Jitihada za Serikali Kupambana na Wizi wa Kazi za Sanaa
Na Raymond Mushumbusi WHUSM
Kilio cha wizi wa kazi za sanaa nchini
kimekuwa cha siku nyingi hali inayosababisha wasanii wengi kukosoa haki ya kazi
zao kwani baadhi ya watu wamekuwa wakitumia kazi zao kujinufaisha wenyewe na
wasanii kubaki wakiwa hawana maendeleo yoyote kutokana na kazi zao ukilinganisha
na wasanii wa nchi jirani za Afrika ya Mashariki na duniani kwa ujumla.
Ikumbukwe katika halfa iliyoandaliwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli kwa
kuwashukuru makundi ya watu mbalimbali wakiwemo wana habari, wasanii na
wanamichezo kwa ujumla Mhe. DKt Magufuli aliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) kusimamia kazi za wasanii na kuhakikisha wanakamata kazi zote ambazo
hazina stika ya TRA.
Katika kutekeleza agizo hilo hivi
karibuni Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye
alifanya zoezi la kushtukiza la kukagua kazi za wasanii ambazo hazina stika ya
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zinakwepa kulipa kodi katika soko la
Kariakoo Jijini Dar es Salaam na kuahidi
kwamba zoezi hilo litafanyika nchi nzima.
Katika zoezi hilo Serikali ilifanikwa
kukamata jumla ya bidhaa za filamu na
muziki 111,802 ambapo 111,529 ni za wasanii wa nje zilizoingia nchini kinyume
na sheria huku bidhaa 273 za wasanii wa ndani zikiwa hazina stika ya ushuru wa
bidhaa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).
Aidha mpaka sasa takribani maduka 42 yamekaguliwa na kukamata mitambo 19 ya kufyatua kazi za wasanii
(duplicators),printer 8 za Cd/Dvd,dvd writers 31,komputa 3,ups 7 kutoka kampuni
ya Aguster.
Katika zoezi hilo Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alisema hatua hii ni ya mwanzo
kwa kuwaonesha watanzania kuwa agizo la Rais wa awamu ya Tano Mhe.Dkt.John
Pombe Magufuli la kulipa kodi na kununua bidhaa halisi kwa kutoa risiti na
kupambana na wizi wa kazi za sanaa nchini linasimamiwa ipasavyo.
Mhe.Nnauye aliongeza kuwa wauzaji
wengi wa bidhaa za filamu na muziki wamekuwa wakikiuka Sheria zinazosimamia tasnia ya Filamu na muziki
ikiwemo sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza na.4 ya mwaka 1976 inayosimamiwa
na Bodi ya Filamu Tanzania.
Waziri Nape Nnauye alizitaja sheria
nyingine kuwa ni Sheria ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na.23 ya mwaka
1984, Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki
na.7 ya mwaka 1999 inayosimamiwa na Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki
( COSOTA) pamoja na Sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147 chini ya kanuni za
stampu kwa bidhaa za Filamu na Muziki ya mwaka 2013 inayosimamiwa na Mamlaka ya
Mapato Tanzania(TRA).
Mhe. Nnauye ameongeza kuwa Serikali
itaendelea kujenga misingi mizuri kwa wasanii na tasnia ya filamu Tanzania na
kuhakikisha wasanii na watayarishaji wanapata mitaji itakayowawezesha kuzalisha filamu bora na kupata masoko
mazuri.
Uchumi wa nchi na wasanii umehujumiwa
sana kwa muda mrefu kufuatia kuwepo kwa
bidhaa za filamu za kitanzania nchini kuuzwa kwa njia zisizo halali na kuikosesha Serikali mabilioni ya fedha
kupitia kodi.
Kwa upande wake katibu Mtendaji wa
Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo amesema wasanii sasa wanatakiwa
kutengenza kazi zenye ubora zaidi ili kuvutia watanzania kununua kazi zao na
kuleta ushindani katika soko la filamu nchini na nje ya nchi.
“ Nawapongeza watayarishaji wa filamu
wanaotemgeneza filamu zenye ubora kwa kuzingatia maadili na wazidi kutengeneza
filamu zenye ubora zaidi ili kukuza tasnia ya filamu nchini na kuongeza pato la
wasanii na taifa” Alisema Bi Joyce.
Bibi. Joyce Fisso ameongeza kuwa Bodi
yake inapokea filamu na maigizo
mbalimbali kwa ajili ya kupata kibali cha kusambazwa hivyo basi jamii
inatahadharishwa kuzingatia kununa filamu zenye stika za TRA katika filamu na
maigizo hayo ili kuepukana wizi wa kazi za sanaa unaozidi kuongezeka siku hadi siku.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. George Haule amewaomba wananchi waunge mkono
jitihada za Serikali kwa kununua bidhaa za filamu zenye stika ya TRA ili kusaidia kuongeza pato
kupitia kodi na kukomesha wale wote wanaokwepa kulipa kodi.
“Nawaomba wananchi waunge mkono
serikali wanunue bidhaa za filamu za ndani na nje zenye stika ya TRA ili
kusaidia kuongeza pato la kodi na la wasanii ili kukomesha wale wote wanaokwepa kulipa kodi”
alisema Bw.Haule.
Baada ya ziara ya kushtukiza ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na
Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye,Chama cha Wasambazaji wa Filamu Tanzania
na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) wamepongeza hatua iliyochukuliwa
na Wizara huyo katika kuhakikisha wanatokomeza waharamia na uuzaji wa kazi za
wasanii bila kufuata utaratibu za kisheria zilizowekwa.
Aidha Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF),Simon
Mwakifamba,amesema kuwa anaunga mkono zoezi linaloendelea kwa wadau wa kazi za
wasanii chini wakishirikiana na Serikali katika kuhakikisha wanatokomeza
uharamia wa kazi za wasanii wote nchini ili walau kuwapa motisha ya maisha
mazuri waigizaji hao ili waendelee kutengeneza kazi nzuri za kuelimisha na
kuburudisha jamii.
Naye Mwenyekiti wa chama cha
wasambazaji wa filamu nchini,Moses Mwanyilu, hayo wakati akizungumza na
waandishi wa habari na kupongeza hatua ya Serikali imekuja katika muda muafaka
kufuatia kilio cha muda mrefu kutokana na baadhi ya wafanyabiashara na
wasambaji wa filamu na muziki kutoka nje ya nchi wamekuwa wakiingiza na kuuza
bidhaa hizo bila ya kufuata utaratibu ikiwemo kulipa kodi.
Amesema kuwa wafanyabiashara hao pia wamekuwa wakidurufu filamu za ndani
ya nchi na kuziingiza sokoni bila ya wasanii kunufaika na kazi zao ikiwemo kazi
hizo kutolipiwa kodi hivyo kupelekea kuziuza kwa bei ya chini ukilinganisha na
filamu hapa nchini jambo ambalo linasababisha soko la filamu za ndani
kudidimia.
Aidha Mwanyilu ameongeza kuwa baada ya kilio cha muda mrefu
hatimaye wameona jitihada za Serikali kupitia kwa Wizara inayohusika na masuala
ya sanaa kuanza kuchukua hatua za makusudi kufanya oparesheni ya nguvu ya
kukamata walanguzi wa kazi za wasanii nchini katika maeneo ya kariakoo.
Naye Katibu Mkuu wa chama cha Wasambaji wa Filamu Tanzania,Suleiman
Ling’ande alisema kuwa tatizo la uharamia katika kazi za wasanii nchini ni
changamoto ya muda mrefu kufuatia kuwepo na sheria ambayo imeshindwa kukidhi na
kusimamia utaratibu unaofaa hasa katika kuhakikisha kazi za wasanii
zinawanufaisha wasanii pamoja na kuliongezea kipato taifa pamoja na kulipa
kodi.
Kwa niaba ya chama cha wasambazaji wa filamu na shirikisho la filamu
Tanzania na vyama vyote vya shirikisho wanapenda kutoa shukrani za dhati kwa
wizara ya habari kupitia waziri wake,Nape Nnauye kwa kushirikiana na mamlaka ya
mapato Tanzania (TRA),Bodi ya filamu,Cosota na Baraza la Sanaa Tanzania kwa
kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kazi za wasanii nchini zinauzwa kwa
kufuata utaratibu uliowekwa na unaotambulika.
Serikali imeahidi kuendeleza zoezi la kukamata bidhaa feki
zinazoingia nchini kinyume na sheria pamoja na zile zinazokwepa kulipa kodi ili
kuinua uchumi wa nchi na wasanii.
Serikali imewahakikishia wasanii na
watengenezaji wa filamu Tanzania kuwa
kazi hii ya kusaka wezi wa kazi za sanaa nchini
itaendelea na haitoshindwa itashinda na imewaonya wanaofanya kazi ya
kuiba kazi za wasanii waache mara moja na yoyote atakayebainika atachukuliwa
hatua kali za kisheria.
Wadau wa sanaa na filamu kwa ujumla wameaswa
kukaa na Serikali na kuangalia namna bora yakuboresha jinsi ya kusambaza kazi
za sanaaa kwa kuzingatia Sheria za nchi na kurasimisha vibanda vinavyoonesha filamu za
kitanzania kuwa kumbi maalum kwa ajili ya kuonesha filamu hizo ili kuongeza
soko la filamu hizo kupitia kumbi hizo.
Post a Comment