Header Ads

JUKWAA HURU LA WAZALENDO TANZANIA latoa Kauli Kuhusu Hujuma Dhidi ya Rais Dkt MAGUFULI

TAMKO JUU YA HUJUMA DHIDI YA MH. RAIS JOHN POMBE MAGUFULI
Dodoma, Mei 8, 2016:

Ndugu wana habari salam,
Mbele yenu ni wajumbe wa Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania, taasisi inayopigania uzalengo na haki ya Watanzania kupata maendeleo bila vikwazo mbalimbali vikiwemo vya kisiasa. 

Tumewaiteni hapa ili kueleza masikitiko yetu juu ya suala moja kubwa hapa nchini lakini lenye vipengele anuai, ambayo ni: hujuma za kisiasa na kiuchumi dhidi ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli na wananchi kwa ujumla.

                             Wanasiasa kumhujumu Rais, Watanzania

Ndugu wana habari,
Kwa miaka mingi mnajua watanzania tulio wengi tumekua tukipiga kelele: tukilia juu ya kero mbalimbali za serikali kushindwa kupambana na watumishi wachache wasio wema wa serikali ambao ni wabadhirifu, mafisadi,wala rushwa,wazembe na wasio na maadili pia wakwepa kodi na wahujumu uchumi. Vita hii tumekua tukipigana sisi watanzania wanyonge na baadaye ikaungwa mkono na makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa.  

Hata hivyo tumesikitishwa kuona baadhi ya wanasiasa na wasomi tuliokuwa nao pamoja katika vita ya kutaka Tanzania yenye neema, sasa tumempata Rais Magufuli anayefanyakazi bila kuchoka kuifikisha Tanzania tunakokutaka, wanasiasa hao wamekengeuka na sasa wanaanza kumhujumu Rais.

Badala ya kumpa moyo na kuungana na Rais katika safari hii ya mabadiliko makubwa ya kifikra na kiutendaji, mabadiliko ambayo yanaungwa mkono na Wananchi na hata Afrika na dunia nzima kwa sasa inajifunza na kusikiliza yanayoendelea kutoka Tanzania, tumeshangazwa zaidi tunaposoma na kusikia katika vyombo vya habari baadhi ya wanasiasa wakianza kumkejeli Rais eti anaendesha nchi kinyume cha sheria na kuipeleka katika utawala wa kiimla.

Ndugu wanahabari,

Hoja hii ni dhaifu na iliyojificha katika hujuma za kutaka kuzuia mageuzi yanayoendelea nchini. Sote tunafahamu kwamba Serikali inamihimili mitatu ya dola ikiwemo Bunge ambalo hivi sasa linaendelea na shughuli zake mjini Dodoma tena wabunge wakilitumia kumtusi na kumkejeli Rais na wananchi waliowachagua. 

Iwapo Serikali hii ni ya kiimla kama wanavyotaka kulaghai wananchi, hata Bunge lisingekaa na baadhi ya wabunge kumkejeli Rais kwa kiwango wanachokifanya.

Sisi watanzania wazalendo tunajua katika serikali inayoendesha utawala wake kiimla (kidikteta) hairuhusu wananchi wake kutoa maoni yao na kuachwa huru kama hawa wanavyotoa maoni yao Bungeni. 

Pia wananchi wanaoadhani wameonewa wanakwenda Mahakamani na mara kadhaa kuishinda Serikali. Ni katika utawala gani wa kiimla utaipata hata hiyo fursa ya kwenda kulalamika Mahakamani?

Tunafarijika kuona kuwa juhudi za Mh za mabadiliko ya kiutendaji sasa zinaungwa mkono hata na viongozi wa vyama vya upinzani wasio na milengo ya kisiasa. Tunatumia fursa hii kutambua hatua madhubuti za “kutumbua majipu” zinazochukuliwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar-es-salaam na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni dhidi watendaji wa serikali wanaokiuka. 

Hawa wanaunga mkono sit u juhudi za Mh Rais bali kiu ya wananchi. Nao waitwe madikteta?

Wahujumu hawa pia wamekwenda mbali na kudai Rais amevunja Katiba na sheria za nchi kwa kuteua na kuwaruhusu mawaziri wake waendelee na kazi bila kuwa na mwongozo (instrument). Hii ni miongoni mwa hoja zao dhaifu za kushadidia ukinzani wao dhidi ya mabadiliko.

Mosi, sisi tunasema nguvu na wajibu wa mawaziri upo kikatiba. Ibara ya 56 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inatamka kuwa Mawaziri na Manaibu Waziri hawawezi kushika madaraka mpaka kwanza waape mbele ya Rais. Mara tu wanapokuwa wameapa wataanza kufanya majukumu yao. Ndivyo alivyofanya Rais Magufuli.

Mwongozo ni waraka tu unaoshadidia mipaka kati ya viongozi na usitumike kisiasa kukejeli kazi kubwa iliyoanza kufanywa na viongozi wetu kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Wajibu wa Mawaziri, yaani, The Ministers (Discharge of Ministerial Functions) Act, Sura ya 299, kifungu cha 5.-(1) kinasema bayana kuwa kutolewa Mwongozo huo sio jambo la lazima. Nanukuu”

“5(1)-The President may, from time to time, by notice published in the Gazette, specify the departments, business and other matters or responsibility for which he has retained for himself or he has assigned under his direction to any Minister and may in that notice specify the effective date of the assumption of that responsibility, and where the President has issued such a notice, it shall, subject to, any subsequent notice issued under this subsection or to any certificate issued under subsection (2) of this section, be conclusive evidence of the matters specified in it.”

Ndugu wanahabari,

Ukisoma nukuu hii, tofauti kabisa na kelele za baadhi ya wanasiasa wasioitakia mema nchi hii wanavyodai, kifungu hiki kama kinavyojieleza hapo juu hakimlazimishi Rais kutoa muundo huo wakati maalum au ndani ya muda maalum bali kinaashiria “kila atakapoona inafaa.”

Kifungu hicho kimetumia neon “may” limetumika na sio “shall” na kisheria tafsiri ya neno “may” limetafsiriwa kama ifuatavyo kwa mujibu wa Black’s Law Dictonary, ukurasa wa 1000, maana yake ni (to be a possibility, yaani ni jambo ambalo kutokea kwake sio lazima). Katika ukurasa wa 1407 neno “shall” lina maana ya “mandatory sense” likiakisi ulazima wa jambo husika.

Ni kwa tafsiri hii rahisi tu iko wazi kuwa Rais halazimiki kwa namna yoyote kutangaza majukumu hayo ila tu kwa utashi wake kama ataona inafaa na kumzongazonga kwa hili ni kukosa hoja. Tunajiuliza kwa kiwango ch usomi wa wanaopotosha kifungu hiki, kuna ajenda gani pana nyuma yaokama si hujuma ambazo hata hivyo zimeshashindwa?

Ni kwa sababu hii, sisi wazalendo tunasema hoja ya baadhi ya wanasiasa na wasomi kung’ang’ania ama Rais analeta utawala wa kidikteta kwa kutumbua majipu au kwamba kwa kuchelewa kutoa mwongozo kwa mawaziri amevunja sheria, tunaona ni si za kisheria wala kizalendo bali zilizojaa hisia binafsi na zaidi ujasiri wa hujuma.

                                        Wafanyabiashara na Hujuma ya Sukari

Ndugu wanahabari,  

Tuhitimishe tamko letu kwa kulaani hujuma nyingine dhidi ya Rais na Watanzania: baadhi ya wafanyabiashara kuficha bidhaa muhimu ya sukari. Tunatumia fursa hii kuwakumbusha wafanyabiashara wakubwa hasa wa sukari, kama ambavyo tumewakumbusha humu pia wanasiasa wanaokengeuka, kuwa waachanae na hujuma hiyo mara moja.

Wanaoendesha uhujumu huo wa uchumi ni sawa na hawa wanasiasa wanaoendekeza hujuma dhidi ya Rais ili asiendeleze mageuzi ambayo ni Watanzania wenyewe ambao waliyataka na wameyasubiri kwa muda mrefu.

Imetolewa na:
Mtela Mwampamba 0627949515/0755178927
Katibu, Jukwaa Huru la Wazalendo Tanzania

No comments

Powered by Blogger.