Mradi wa Ng'ombe Kuwanufaisha Wanawake wa Vijijini Wilayani NGORONGORO

  Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Hashim Mgandilwa akiongea na wakazi wa Ngorongoro wakati wa kukabidhi Ng'ombe hao.
 Robert Kamakia kutoka shirika la PALISEP akimkabidhi Mkuu wa Wilaya Mhe. Hashim Mgandilwa risala kuhusu makabidhiano hayo. 
 Theresia Irafay, Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Ngorongoro akizungumza wakati wa ugawaji wa Ng'ombe hao.
 Laurent Wambura kutoka shirika la Oxfam akizungumza wakati wa ugawaji wa Ng'ombe hao.
Mh. Hashim Mgandilwa, Mkuu wa wa Wilaya ya Ngorongoro akikabidhi Ng'ombe kwa wanawake wa wilaya ya Ngorongoro.
 Wakazi wa vijiji vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu Juu wakihudhuria ugawaji wa Ng'ombe uliofanyika katika kijiji cha Enguserosambu. 
 Picha ya pamoja.
..................
..................
Wanawake
 wenye kipato cha chini kutoka vijiji vinne vya wilaya ya 
Ngorongoro wamekabidhiwa Ng’ombe ili kuwasaidia kuondokana na umasikini.
Wanawake
 hao wapatao 28 kutoka vijiji vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu 
Juu walichaguliwa kulingana na hali yao ngumu ya maisha inayowapelekea 
wakati mwingine kunyanyaswa kijinsia kupitia mfumo dume. Wanawake 
wengine 15 watakabidhiwa Ng’ombe wao mnamo mwezi Machi mwaka huu kufanya
 idadi ya wanufaika kufikia 43.
Makabidhiano
 hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Enguserosambu yalihudhuriwa na  
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, viongozi mbalimbali wa vijiji, pamoja na 
wakazi wa eneo hilo.
Akikabidhi Ng’ombe hao Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Hashim Mgandilwa 
aliwataka wanawake hao kuhifadhi vizuri mifugo hiyo ili iwasaidie 
kujikwamua kiuchumi kwa kuuza bidhaa zitokanazo na Ng’ombe ikiwemo 
maziwa. Aidha Mkuu huyo wa wilaya alitoa rai kwa viongozi wa vijiji 
hivyo kuhakikisha kwamba inapotokea misaada kama hii iwanufaishe 
walengwa ambao mara nyingi ni watu maskini ili kuwaepusha na balaa la 
njaa.
Ng’ombe hao wametolewa kama msaada na shirika la Oxfam kupitia wadau wake shirika la PALISEP.
Akizungumza
 katika hafla hiyo Meneja wa programu ya wafugaji wa Shirika la Oxfam 
ndugu Laurent Wambura alisema shirika lake limefanya hivi ili kuwainua 
kiuchumi wanawake wenye kipato cha chini na kubadilisha mtazamo wa jamii
 ione kwamba hata wanawake wanaweza kumiliki mali ikiwemo mifugo na 
kubadilisha kabisa maisha yao.
Naye
 Mkurugenzi wa shirika la PALISEP Robert Kamakia alisema lengo la mradi 
huo ni kuwezesha upatikanaji wa lishe bora na maziwa kwa familia zisizo 
na uwezo pamoja na kupunguza makali ya magonjwa kwa watoto kama vile 
utapiamlo.
Hii
 sio mara ya kwanza kwa shirika la Oxfam kugawa Ng’ombe katika wilaya ya
 Ngorongoro, mnamo mwaka 2014 wanawake wapatao 66 walinufaika na mradi 
huu kwa kugawiwa ngo’mbe mmoja jike kila mmoja huku viongozi wa vijiji 
vinne vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu Juu wakikabidhiwa madume
 6 wa mbegu kama sehemu ya kuboresha mifugo ili kukidhi mahitaji ya 
soko. Ndama wote wanaozaliwa kama uzao wa kwanza wa Ng’ombe hawa 
hugawiwa kwa wanawake wengine wenye kipato cha chini hivyo kunufaisha 
jamii kubwa.









Post a Comment