Kada wa CCM Salum Hapi Apongeza Uteuzi wa Mama MIGIRO
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Joseph Magufuli amefanya uteuzi wa Mabalozi watatu kwa ajili ya kuwakilisha nchi yetu katika Balozi zetu nje ya nchi.
Katika majina yaliyoteuliwa ni pamoja na Dr. Ramadhani Dau, Dr. Asha-rose Migiro na Mathias Chikawe. Sio kusudio langu kuwazungumzia mh. Chikawe na Dr. Dau kwa leo. Lakini hili la Dr. Asha-rose Migiro nimeshawishika kuchukua kalamu na kuandika.
Msukumo mkubwa ulionifanya kuchukua kalamu yangu na kuandika umetokana na mazungumzo ya watu mbalimbali pamoja na makala tofauti zilizoandikwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari juu ya "Dr. Migiro amepanda au ameshuka"?
Wengine wakaenda mbali zaidi kujiuliza kama kwa nafasi alizowahi kushika anastahili kuteuliwa Balozi au la. Mbali na maswali haya ya ufahamu, wapo walioamua kuandika makala. Makala hiyo ambayo binafsi nachelea kuifananisha na hekaya za abunuwasi imejaa dhana zisizo na mifano na ushahidi wowote wa kidiplomasia zinazoelezea kukosoa uteuzi wa Rais Dr. John Pombe kwa Dr. Asha-rose Migiro. Nimeamua kuandika ili kutoa elimu na kusahihisha hekaya hizo za abunuwasi.
Katika medani za diplomasia duniani, Balozi ni muwakilishi wa Raisi katika nchi husika aliyopangiwa kuwakilisha. Pamoja na ukweli kwamba shughuli za Mabalozi zinaratibiwa na wizara ya mambo ya nje kiutendaji, lakini mamlaka ya uteuzi na hata utenguzi wa Balozi yako kwa Raisi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Dr. Asha-rose Migiro amewahi kuwa Waziri wa wizara mbalimbali ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ikiwemo wizara ya mambo ya nje. Pia amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa - UN kabla ya kumaliza muda wake na kurejea nchini ambako hata hivyo aliteuliwa tena kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Nafasi zote hizi alizowahi kushikilia Dr. Migiro hazizuii yeye kuteuliwa kuwa Balozi kama alivyofanya Mh. Rais Dr. Magufuli.
Hakuna makosa yoyote ya kisheria, kiitifaki wala kidiplomasia katika kumteua mtu wa nafasi ya Dr. Migiro kuwa Balozi. Binafsi ningeshangaa sana kama Dr. Migiro angekataa uteuzi huo wa Rais Magufuli.
Katika medani za diplomasia duniani wako viongozi mbalimbali wakubwa ambao baada ya kustaafu madaraka makubwa ya serikali nchini mwao walipata kuteuliwa kuwa Mabalozi kuwakilisha nchi zao katika mataifa mengine.
Nitatoa baadhi ya mifano ili kusaidia kushibisha hoja zangu. Katika nchi yetu wako mawaziri waandamizi wakubwa waliowahi kushikilia nyadhifa kubwa serikalini ambao baada ya nyadhifa hizo walipata teuzi za Raisi za kuwa Mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali.
Waheshimiwa hawa ni kama mh. Mwinyi, mh. Benjamin Mkapa, mh. John Samuel Malecela, mh. Balozi Mwakawago, Balozi Mongella, balozi Job Lusinde, mh. Balozi Wilson Masillingi, mh. Balozi Philip Marmo na mh. Balozi Mustafa Nyang'anyi.
Viongozi hawa wastaafu walikua mawaziri waandamizi na wengine wakihudumu wizara ya mambo ya nje. Lakini baadae katika nyakati tofauti wote walipata teuzi za Rais kuwa Mabalozi. Nchini Afrika kusini, aliyekua Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo comrade Nqakula aliteuliwa kuwa Balozi wa Afrika Kusini nchini Msumbiji.
Marekani ilimteua Jenerali Mstaafu wa jeshi Balozi Alphonso Leinhard kuwa balozi wa Tanzania baada ya kuwa ameshika wadhifa wa Jenerali katika jeshi la Marekani.
Hapa nchini Tanzania majenerali wa jeshi wamewhi kuteuliwa kuwa Mabalozi katika vipindi na nchi tofauti. Hao ni pamoja na CDF mstaafu Balozi Meja Jenerali Mirisho Sarakikya, Balozi Meja Jenerali Silas Mayunga aliyekuwa Nigeria na Mnadhimu Mstaafu wa JWTZ Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Abdulrahman Shimbo aliyeteuliwa kuwa balozi nchini China. Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliteuliwa na Raisi wa nchi hiyo kuwa Balozi wao nchini Afrika Kusini.
Hoja ya kuwa Dr. Migiro alikua Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa - UN na hivyo hastahili kuteuliwa kuwa Balozi ni hoja dhaifu sana katika diplomasia. Kwanza Umoja wa Mataifa ni taasisi, na Tanzania ni nchi huru yenye watu, mipaka na serikali yake. Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa ni kubwa katika ngazi ya taasisi hiyo ya UN, lakini Dr. Migiro anaporudi ndani ya nchi yake ya Tanzania, itifaki ya nchi inaanza na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan anapokuwa nchini kwake Ghana, anakua raia kama raia wengine wa Ghana na hawezi kuwa juu ya Raisi wa nchi katika itifaki. Hivyo huwezi kulinganisha uteuzi wa Rais Magufuli wa Balozi Migiro na uteuzi wake kuwa Naibu Katibu Mkuu wa taasisi (UN).
Ndio maana pamoja na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN, Dr. Migiro hakuitwa Balozi, maana cheo cha Balozi wa nchi anaweza kukitoa Rais wa nchi peke yake. Na sasa nchini kwenu ni Raisi Magufuli pekee ndiye mwenye mamlaka ya kikatiba na kisheria kumteua mtu kuwa Balozi.
Pili, kutumika kwa Dr. Migiro katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa hakuizuii nchi yake kumtumia katika jukumu lingine lolote ambalo nchi itaona anaweza kusaidia.
Ndio maana baada ya kurudi nchini Dr. Migiro aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na ndani ya CCM akateuliwa kuwa Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI). Kwa hoja hizo Rais Dr. Magufuli hakukosea katika kumteua Dr. Asha-rose Migiro kuwa Balozi na wala Dr. Migiro hatakuwa na kosa lolote kupokea uteuzi huo.
Ni heshima kubwa kuona kuwa mchango wako unahitajika katika kumsaidia mh. Raisi. Pia ni heshima kubwa kuendelea kuitumikia nchi yako katika nafasi kubwa ya Balozi. Wale waliodhani kuwa mh. Raisi Dr. John Magufuli kakosea wanapungukiwa elimu ya diplomasia.
Kadhalika wale waliodhani kuwa Dr. Asha-rose Migiro alipaswa kukataa uteuzi huu hawajui maana ya Balozi na pengine makala hii itawasaidia kupata elimu na kuweza kutofautisha kati ya taasisi na nchi.
Hata Katibu Mkuu wa UN Ban Ki Moon akistaafu nafasi yake ndani ya Umoja wa Mataifa anaweza kuteuliwa na nchi yake kuwa Balozi. Dr. Migiro na wenzake walioteuliwa na Raisi Magufuli kuwa mabalozi katika itifaki na diplomasia wamepewa heshima kubwa na wanapaswa kujipanga kutekeleza majukumu yao vema ili waweze kulinda heshima waliyopewa na taifa lao.
Nawaasa wale wasioelewa mambo watumie muda wao kusoma na kufanya tafiti kabla ya kuamua kukosoa.
Imeandikwa na Comrade, Ally Salum HAPI
Post a Comment