Jaji Mkuu wa KENYA Dkt WILLY MUTUNGA asifu Utendaji wa Mahakama ya TANZANIA
Jaji Mkuu wa Kenya Mhe.
Dkt. Willy Mutunga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa utendaji wake wa kusikiliza na kuamua mashauri mengi
yanayopelekwa mahakamani. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman na Kulia ni Jaji Kiongozi Mhe. Shaan Lila.
Jaji Mkuu wa Kenya Mhe.
Dkt. Willy Mutunga (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuipongeza
Mahakama ya Tanzania kwa utendaji wake wa kusikiliza na kuamua mashauri mengi
yanayopelekwa mahakamani. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande
Othman na Kulia ni Jaji Kiongozi Mhe. Shaan Lila.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu ujio wa Jaji Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Willy Mutunga
na jinsi Mahakama ya Tanzania ilivyonufaika na ujio wake. Februari 4 mwaka huu
Tanzania itaadhimisha Siku ya Sheria.
Na.
Aron Msigwa – Dar es salaam
Jaji Mkuu wa Kenya Mhe.
Dkt. Willy Mutunga ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa utendaji wake wa
kusikiliza na kuamua mashauri mengi
yaliyopelekwa mahakamani kwa mwaka wa sheria uliopita wa 2015 na kutoa wito kwa
watendaji wa Mahakama ya Tanzania kuendelea kufanya vizuri licha ya changamoto
mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Jaji Mkuu wa Kenya ametoa
pongezi hizo mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam mara baada
ya kukutana na kufanya mazungumzo na Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya
Rufani wa Mahakama ya Tanzania kufuatia mwaliko alioupata wa kuhudhuria
maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yatakayofanyika Februari 4 mwaka huu.
Mhe. Dkt. Mutunga amesema
kuwa nchi ya Kenya mpaka sasa ina
mashauri yapatayo 300,000 ambayo bado hayajaamuliwa na kuongeza kuwa asilimia 5
ya wananchi wa Kenya ndio hupeleka mashauri yao Mahakamani huku asilimia 95 iliyobaki
wakitafuta ufumbuzi wa kesi zao nje ya Mahakama.
“Ni kweli Tanzania
mnafanya vizuri katika katika kusikiliza mashauri kwa haraka, asilimia 95 ya
Wakenya hutafuta ufumbuzi wa kesi zao kwa viongozi wa kidini na Kimila kutokana
na baadhi yao kukosa fedha za kutosha za kufuatilia na kugharamia kesi zao”
Amesema.
Ameongeza kuwa Mahakama
ya Kenya kwa mwaka huu 2016 imejipangia malengo ya kuhakikisha kuwa
inasuluhisha mashauri yote ndani ya mwaka mmoja ili kuongeza ufanisi na imani
kwa wananchi.
Ameeleza kuwa Tanzania
ina jambo la kujifunza kutoka Kenya kufuatia mageuzi ya Katiba iliyoyafanya
mwaka 2010 hususan kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo na nafasi ya Mahakama kwenye
Katiba Mpya ambayo Tanzania inaendelea na mchakato wake.
Akizungumzia mageuzi hayo
ambayo tayari Kenya imeyafanya kufuatia kuwepo kwa Katiba mpya Mhe. Mutunga
amesema kuwa ni pamoja kupungua kwa madaraka ya Rais katika kuteua Majaji, na
nafasi za Majaji kutangazwa na watu kupeleka maombi na sifa zao kujadiliwa
ambapo wananchi huruhusiwa kutoa maoni kwa Tume ya Mahakama ya Kenya kuhusu
majaji hao kabla ya kuapishwa.
Aidha, ameeleza kuwa
Watanzania wana kila sababu ya kujivunia umoja na mshikamano uliopo ambao
umesababishwa na waasisi wa taifa hilo huku akibainisha kuwa majadiliano na
upatikanaji wa Katiba Mpya nchini Tanzania utafanywa na Watanzania wenyewe kwa
ufanisi mkubwa kwa kuwa Watanzania ni walimu na mfano wa kuigwa katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki na Bara la Afrika.
Kwa upande wake Jaji Mkuu
wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman akizungumzia ujio wa Jaji Mkuu wa Kenya
amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imenufaika na ujio wake kwa kuwa iko kwenye
maadhimisho ya Wiki ya Sheria ambayo huwakutanisha wadau mbalimbali wa sheria
kujadili changamoto na mafanikio ya Sekta ya Sheria nchini.
Amesema kufuatia ziara ya
Jaji Mkuu wa Kenya Mhe. Dkt. Mutunga Mahakama ya Tanzania imejifunza masuala
mbalimbali ambayo ni muhimu katika ufanisi wa shughuli zake ikiwemo uboreshaji
wa Maslahi ya Watumishi wa Mahakama, Jukumu la Mahakama kutafsiri Katiba kwa
kuangalia historia, uchumi pamoja uanzishwaji wa utaratibu wa kuazima baadhi ya
hukumu zilizotolewa nchini Kenya kama ushauri.
Aidha, amesisitiza
kuwa Mahakama ya Tanzania inao wajibu wa kuendelea kuongeza uwazi katika
upatikanaji wa watendaji wenye nia ya kuwatumikia
wananchi pamoja na kuboresha njia za kuwapata majaji wa Mahakama
ili kuongeza ufanisi.
Post a Comment