DINA SAMANYI "Miaka 39 ya CCM makada Watulie Ndani ya Chama"
Dinah Somba Samanyi ambae ni Katibu wazWazazi (CCM) Mkoani Mwanza.
Na:George Binagi
Ikiwa hii leo ni Maadhimisho ya Miaka 39 tangu kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM, Wanachama wake wametakiwa kutulia ndani ya Chama hicho badala ya kujitoa katika chama jambo ambalo huwafanya baadae kujutia.
Kauli hiyo imetolewa Mkoani Mwanza na Katibu wa Wazazi wa Chama hicho Ndg.Dinah Somba Samanyi, wakati akizungumza na BMG, kuhusiana na maadhimisho ya miaka 39 ya CCM mwaka huu 2016.
Samanyi ametanabaisha kwamba, mwaka huu ikiwa ni miaka 39 tangu CCM kuasisiwa February 05,1977 ikiwa ni baada ya Muungano wa wa vyama viwili vya ASP kutoka Zanzibar na TANU kutoka Tanganyika, ni vyema wanachama wake wakawa waadilifu na kuepukana na tabia zisizo za kimaadili ambazo ni pamoja na kujitoa ndani ya chama hicho kama ambavyo baadhi yao wameshuhudiwa wakifanya jambo ambalo hata hivyo huwafanya baadae kulijutia.
Kuhusu maadhimisho amesema "Chama kimejipanga vizuri katika kuadhimisha Siku hii na tangu kuzinduliwa Kitaifa kwa sherehe za maadhimisho haya kule Zanzibar, kumekuwa na shughuli mbalimbali zinazolenga kuimarisha uhai wa chama pamoja na kushiriki shughuli tofauti tofauti za kijamii".
Samanyi amebainisha "Katika Mkoani Mwanza kila Wilaya imepewa fursa ya kuandaa shughuli mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho haya. Jumuiya mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Wazazi zimeshiriki shughuli tofauti tofauti kama vile kutembelea mashuleni, kufanya usafi wa mazingira pamoja na kutembelea wagonjwa Mahospitalini".
Nao baadhi ya makada wa vyama vya siasa Mkoani Mwanza wametoa maoni yao kuhusiana na miaka 39 ya CCM kikiwa ni chama kinachoongoza Serikali, ambapo Kada wa CCM Sarah Ramadhan anasema anasema kuwa miaka 39 ya chama hicho, taifa limepiga hatua kubwa kimaendeleo ikilinganishwa na miaka iliyopita huku Amos Joseph ambae ni Kada ya Chadema akisema kuwa miaka 39 ya uongozi wa CCM taifa limeshindwa kutatua changamoto za kimaendeleo ikizingatiwa kwamba maendeleo yaliyopatikana hayaendani na raslimali za asili zilizopo nchini.
Pengine Maoni ya Makada hao ni fursa nyingine ya kuiwezesha CCM kuzidi kuwatumikia vyema Watanzania ili miaka 40 ijayo mwakani kusiwepo na utofauti wa kimtizamo pindi makada wa vyama vya siasa watakapokuwa wakitoa tena maoni yao.
Kitaifa Sherehe za Miaka 39 ya Kuasisiwa Chama cha Mapinduzi CCM kwa mwaka huu, zilizinduliwa Visiwani Zanzibar na Dkt.Ali Mohamed Shein ambae ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa na kilele chake kinahitimishwa Mjini Singida katika Uwanja wa Namfua ambapo zitahitimishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.
Post a Comment