Header Ads

Wananchi Waaminifu wasaidia Viongozi wa Vijijji Kuchukua Hatua na Kujua Wajibu wao wa Kazi

Mraghbishi Zaituni Rashida toka wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga.

...............................


Katika vijiji vya mikoa ya Geita, Simiyu, Shinyanga na Arusha, wananchi wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanajisimamia wao wenyewe na viongozi wao ili kufanikisha shughuli za maendeleo. Hata hivyo, si wote wanaofanya hivyo. 

Wale walio mstari wa mbele tunawaita waraghbishi na kile wanachofanya ni uraghbishi, Hawa ni wale wanaochukua hatua kustawisha au kulinda haki za binadamu na maslahi ya jamii kwa ujumla wake; kiuchumi, kisiasa au kijamii. 

Watu hawa wapo kwenye makundi tofauti tofauti wakiwamo wenyeviti wa vijiji, madiwani, wakulima, wafugaji, viongozi wa kidini, sungusungu, na walimu. Watu hawa wamechukua hatua mbalimbali ikiwamo kuwashawishi na kuwawezesha wanavijiji wenzao kuwa waraghbishi. Uraghbishi wao kwa wenzao unafanyika kwa njia mbalimbali; iwe kwa kukutana kwenye vijiwe vya kahawa, mashambani, kwenye visima vya kuchotea maji, shuleni ama popote pale wanapopata nafasi zikiwamo sehemu za ibada.

Harakati hizi zimewawezesha kujisimamia kwa kutambua wajibu na haki zao wanazostahili kuzidai kutoka, aidha kwa viongozi wao waliowachagua ama wale waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali kwa niaba yao. Mifano ipo mingi kuanzia kudai taarifa na mapato na matumizi, kudai huduma bora za kijamii kama upatikanaji wa dawa kwenye zahanati, huduma za maji na elimu n.k.Pamoja na mafanikio hayo, bado ni jukumu la uraghbishi si rahisi. 

Ni gumu na linalokatisha tamaa. Waraghbishi hawalipwi malipo yoyote zaidi ya kutumia zaidi walichonacho, kubwa zaidi likiwa ni muda wao. Ni shughuli ambayo wakati mwingine yaweza kukutia matatizoni.


Hakuna mtu anayependa kufuatiliwa mambo yake, hasa yanapokuwa na matatizo;

 yawe ya kujisababishia au ya bahati mbaya. Uraghbishi ni pamoja na kumulika mambo ambayo yanawahusu watu wengi. Akieleza changamoto ya kufanya uraghbishi, Melina Ndumuzi, toka wilayani Mbogwe mkoani Geita anasema: “Yataka moyo wa ujasiri sana kufanya uraghbishi vinginevyo unaweza ukaogopa kuthubutu. 

kwa sababu ya mtazamo wa jamii kuhusu watu waraghibishaji.” Kwa upande wake Epifania Mwenda toka kijiji cha Tanga, kata ya Katente wilayani Bukombe anasema:

“Maisha ya uraghbishi ni ya kujitolea zaidi, si rahisi ni kazi sana, njia pekee ni kupenda kufanya unachofanya. Matokeo ya kile unachofanya ndio utaona mwisho wa siku wengine wanavutika kuraghbisha. Ila ni kazi nzito na kama una moyo mdogo huwezi kuifanya.”

Zaituni Rashid anayefanya uraghbishi katika kijiji cha Mhunze, kata ya Kishapu, mkoa wa Shinyanga anataja changamoto ya kukimbiwa na wale anao waraghbisha, “Huku kwa ujumla tunajitolea, inafika mahali wenzako wanakukimbia kila mmoja ana sababu zake, yaani shidaa!” Ugumu unakuja hasa pale unapokuwa ni mwajiriwa wa serikali na wakati huo huo unafanya uraghbishi. Kwa mfano mraghbishi ambaye ni mwalimu na kwa upande mmoja anawaunga mkono wale wanaopingana na mwenendo wa mkurugezi wa wilaya, ambaye ndiye mwajiri wake. 

“Ebu fikiria unamuona mwenzako anatafutwa na mwajiri wako, na wewe upo upande wa mraghbishi. Ni changamoto sana,” anaeleza mraghbishi William Msangi toka kijiji cha Buluhu kilichopo kata ya Ipoja wilayani Mbogwe. 

Akiunga mkono changamoto hiyo ya kimaslahi Zaituni Rashida anasema, “Sisi huku ni shida, mapato yanaliwa na wakuu wako. Unaanzaje kuwasonga? Na ukiwahoji viongozi wa chini wanakueleza kwenda kwa mkurugenzi wako,” Said Simoni toka kijiji cha Mheza, yeye kwa upande wake anaanza kwa kuuliza waraghbishi wenzake toka vijiji vya wilaya yao Bukombe kuhusu uragbishi wao katika vijiji vyao. 

Swali hili anawauliza baada ya kukutana na wenzake“Vipi vikao vya wazazi mashuleni vimefanyika nyie huko kwenu.?”Swali hili anauliza akilinganisha na changamoto zinazokabili uraghbishi katika eneo hilo na kamati za shule za vijijni. Kamati hizi zinaundwa na watu 9; Diwani (1), walimu (3) na wazazi (5). Mwenyekiti wa kijiji anakuwa kama mgeni mwalikwa.


Mraghbishi William Msangi toka kijiji cha Iponya, wilaya ya Mbogwe, mkoani Geita.

....................................

Akiongelea changamoto anazokumbana nazo hasa linapokuja suala la kusimamia kamati za shule, Simon anasema:“Yaani hadi mtu anafikia mahala anasema unataka uchukue cheo chake, kisa nimeuliza maswali yanahusu mapato na matumizi ya shule. 

Ni ngumu sana kwa sababu wabadhirifu hawapendi sana kufuatwafuatwa. 

Hivyo, muda mwingine unajikuta upo kwenye mtafaruku usioutarajia.”Hofu hii ya wananchi kuuliza maswali kwa viongozi waliowachagua ni chagamoto. 

Simon anaongeza kwa kusema: “Elimu inahitajika mno ili watu waweze kujiamini kwani kuna watu wanawasujudia madiwani kama miungu watu wakati wao ndio waliomweka madarakani. Hali hii ya kuwaogopa viongozi ni tatizo kubwa.”

Na hapo ndipo wanapokiri kuna umuhimu wa kuwa na mbinu mbadala ya kufanya uraghbishi, vinginevyo waraghbishi na wale raia waamilifu ambao ni waajiriwa na muda huo huo ni wananchi hujikuta katika mazingira hatarishi. 

Na hawa viongozi wa chini wanahitaji kupatiwa mbinu za uraghbishi. Kwa nini? Kwa sababu kuna baadhi yao wana hofu na woga kwa wakubwa zao.


Hatua mbalimbali wanazochukua zinatokana na uamilifu wao; yaani uwezo wa kujitambua na kusimamia kile ambacho wanaamini sahihi. Kwa kufanya hivyo wanakuwa si tu waraghbishi bali pia raia waamilifu. Pamoja na changamoto hizo, na nyingine nyingi kama za kutishiwa kufungwa au kudhuriwa, bado raia hawa waaminifu wameendelea na uamilifu wao. Akifafanua nini hasa kinachowasukuma kufanya uraghbishi, Gabriel Jonathan toka kijiji cha Lugunga anasema: 

“Watu hawa ni wa muhimu na mafanikio ya uraghbishi ni kuungwa mkono na watu wengi. Hapa changamoto lazima iwe inahusisha watu wengi, hiyo ndio tunaiita changamoto.” Ili mtu aweze kuchukua hatua ni lazima awe na sababu inayomgusa. 

Mraghbishi unapoibua jambo ni lazima uwe umelifanyia tathmini ya kutosha na kujiridhisha kwamba unachowaambia watu ni sahihi. 

Watu ni changamoto ambayo inaendana na muda. Waraghbishi wengi ni watu ambao wana shughuli zao. Na shughuli hizi ndizo zile zinazowaingizia kipato wanachotumia na familia zao. Akifafanua changamoto hii baba wa watoto wanne na mke, Gabriel Jonathan anasema:


“Ili waweze kuchukua hatua ama kufanya kitu fulani, wanahitaji uwepo wako. Wasipokuona kwenye vikao hivyo huwa inawakatisha tamaa, hivyo inakulazimu kufunga biashara na kuja kujumuika na watu. Hii ni changamoto kubwa.”Unahitajika ubunifu mpya wa kuwawezesha waraghbishi kukabiliana na changamoto hizi. 

Njia mojawapo ni kutengeneza urafiki na wale ambao tunahitaji kuwabadilisha. Njia hii ni muhimu katika kushawishi wale ambao kwa njia moja ama nyingine wanaoneka kwenda kinyume na maadili ya uongozi. 

Kwa kufanya hivi inasaidia kupunguza uhasama na kuonana kama maadui.  Akisisitiza umuhimu wa dhana ya nguvu, Richard Mabala anasema waraghbishi wakumbuke daima kwamba nguvu yao hutokana na nguvu ya watu na si mapambano binafsi. Na hii ndio siri ya mafanikio ya waraghbishi ama raia waamilifu. 

Kwa kawaida wajumbe wengi wa halmashauri ya serikali ya kijiji hutegemea posho za vikao kama njia mojawapo wa kujikimu. Hawa hawana mshahara na ni watu kutoka kwenye jamii ile ile ya wale waliowachagua. Ni mara chache sana wanaunga mkono hoja ya kutolipwa kwenye vikao.


Kutokana na uraghbishi, wajumbe wa kijiji cha Buluhe kilichopo kata ya Iponya walikubaliana kutopokea fedha za posho na badala yake zitumike katika shughuli nyingine. Akielezea jinsi alivyowabadilisha wajumbe wa halmashauri ya kijiji kuwa raia waamilifu, katika maana ya kujitambua, William Msangi toka anasema: 

“Baada ya kuwaraghbisha wajumbe wa halmashauri ya serikali ya kijiji kuhusu dhamana yao kwa wananchi kwa kuacha kujitazama wao wenyewe zaidi, walikubali kutopokea posho. 

Kwa siku hiyo tuliweza kuokoa kiasi cha shilingi laki tatu na elfu sabini na tano,” Baada ya fedha hizo kukusanywa zilikabidhiwa kwa mwenyekiti wa kamati ya mipango na fedha ikiwa kama ni sehemu ya uraghbishi kwani hapo mwanzo fedha alikuwa anakaa nazo mtendaji wa kijiji, jambo ambalo halikuwa sahihi. 

Kwa hiyo ili uamilifu na uraghbishi uwe wa kweli inabidi liwe ni suala la watu na si la mtu mmoja mmoja ili nguvu za pamoja zifanye kazi. Na hapo ndipo ujenzi wa taifa unapoonekana moja kwa moja kwa sababu ni chetu si sote. Pamoja na changamoto zote bado raia hawa waamilifu wamendelea na harakati za ujenzi wa taifa pasipo kukata tamaa na badala yake wanaendelea kuhamasishana wao kwa wao.  

No comments

Powered by Blogger.