Rais Dkt JOHN MAGUFULI awaonya Wakuu wa Mikoa na Wilaya Kuhusu Baa la Njaa
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameonya kuwa wilaya ama Mkoa
wowote ambao utakumbwa na njaa, itakua ni kipimo tosha cha kuonesha kuwa Mkuu
wa Mkoa ama Mkuu wa wilaya husika hafai kuendelea na wadhifa huo.
Rais Magufuli
ametoa onyo hilo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti aliposimamishwa na
wananchi wa Arusha Mjini akiwa njiani kuelekea Monduli ambako amefunga za "Zoezi Onesha Uwezo Medani" lililoandaliwa
na kutekelezwa na kamandi ya Jeshi la nchi kavu ambalo ni sehemu ya jeshi la
wananchi wa Tanzania.
Amesema kwa kuwa
mvua zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, Viongozi wa Wilaya
na Mikoa wana wajibu wa kuwahamasisha wananchi kuzalisha mazao ya chakula ili
wasikumbwe na njaa.
Rais Magufuli
ameendelea kuwasihi wananchi wa Arusha Mjini kuwa uchaguzi umekwisha na kwamba
kilichobaki sasa ni kazi huku akiwahimiza kufanya kazi za uzalishaji mali
ikiwemo kilimo.
"Naomba ndugu
zangu mniombee, na ninapenda kuwahakikishia kuwa sitawaangusha. Yote
niliyoahidi nitayatekeleza bila kubagua nawaombeni mnipe muda na muwe
wavumilivu" alisisitiza Rais Magufuli.
Amerejea kauli
zake alizozitoa jana alipoingia mkoani Arusha kuwa atendelea kuwashughulikia
wezi, mafisadi na watendaji wote wa serikali ambao wamekua wakijineemesha kwa
kufuja mali ya umma kupitia kampeni yake ya "Kutumbua Majipu" na
amewaomba watanzania wote waendelee kumuombea ili atumbue majipu yote hadi yaishe.
Rais Magufuli amelazimika kuzungumza na
wananchi wa Arusha Mjini waliokuwa wamekusanyika kwa maelfu kando kando mwa
barabara na hivyo kujikuta akisimamishwa na wananchi wa Sanawali, Tekniko, Ngarenaro, Kona Ya Nairobi, Mbauda, Majengo Na
Kisongo.
Akiwa katika eneo
la Ngarenaro wananchi wamelalamikia vitendo vya rushwa vilivyokithiri katika
mahakama ya mwanzo ya Maromboso na pia katika eneo la Kona ya Nairobi wananchi
wamelalamikia kero za kelele na uchafu wa kiwanda kilichojengwa kandokando mwa
barabara ambapo Rais Magufuli ameahidi kufanyia kazi kero hizo.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha.
22
Januari, 2016.
Post a Comment