Header Ads

Shindano lenye Fursa ya Kukuza Mitaji kwa Vijana lazinduliwa

DSC07284-2
Mwenyekiti wa Taasisi ya MO Dewji, Mohammed Dewji.


Na Modewjiblog team

Mwenyekiti wa Taasisi ya MO Dewji, Mohammed Dewji kwa kushirikiana na kampuni ya Darecha Limited leo (jumatatu) wamezindua shindano la Mo Mjasiriamali lenye lengo la kusaidia kukuza ujasiriamali miongoni mwa vijana.

Shindano ya Mo Mjasiriamali litatoa fursa ya ukuzaji wa mitaji, ulezi wa wajasiriamali na mitandao ya biashara kuongeza mwanga, ujasiri na kuzalisha wajasiriamali Tanzania.

“Mimi kama Mjasiriamali kijana na mzaliwa wa Singida vijijini, sikufikiria hata mara moja kama leo ningekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa moja ya makampuni yaliyofanikiwa sana katika nchi yetu na hata barani Afrika.” Inasema taarifa Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MeTL kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki.

Aidha alisema Afrika ni moja ya bara linalokua kwa haraka na lenye ukuaji imara wa uchumi na amini vijana wa Tanzania wana nafasi kubwa ya kutumia fursa hizo ili kujiletea uchumi endelevu.

Lakini pamoja na ukweli huo changamoto kama za ukosefu wa mitaji, ukuzaji ujasiriamali na mitandao ya biashara zimekatisha tamaa vijana wengi kukuza kwa mafanikio makampuni yao hapa Tanzania na hivyo kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa watu wa kipato cha kati.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Benki ya maendeleo ya Afrika (ADB), watu wenye kipato cha kati katika bara la Afrika wataongezeka na kufikia watu bilioni 1.1 ifikapo mwaka 2060.

Watu wa kipato cha kati ndio wanaochagiza ukuaji wa uchumi kutokana na mahitaji yao na pia ari ya ujasirimali.

Pamoja na ukweli huo kunachangamoto nyingi zinawakabili watu hao wa kipato cha kati. Mathalani nchini Tanzania changamoto kubwa kwa vijana wajasirimali ni gharama za kutafuta mtaji kwa kazi hizo.

“Kuna haja kubwa ya kuhakikisha kwamba vijana hawa wanaondolewa tatizo la ujasirimali ili waweze kusukuma mbele uchumi wa Tanzania.” inafafanua taarifa hiyo.

Aidha kwa kuwa Tanzania inaelezwa kuwa ni nchi ya 19 katika bara la Afrika kuhusiana na fursa na ujasirimali ipo haja ya kusaidia ili kuiondoa katika nafasi hiyo. Taarifa ya nafasi ya Tanzania imo katika ripoti yake ya mwaka 2014 ya Africa Prosperity Report.

Taarifa ilifafanua zaidi kwamba kutokana na haja hiyo Taasisi ya Mo Dewji na Darecha Limited wameungana pamoja na kuanzisha shindano la Mo Entrepreneurs ili kutambua na kuuenzi mchango wa wajasirimali chipukizi na kufanikisha ndoto zao.

Ili kufanikisha nia ya kuwa na wajasiriamali wengi, shindano hilo linatarajiwa kuwa daraja kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji, Mohammed Dewji (MeTL Group na Mwenyekiti wa Mo Dewji Foundation) ambapo vijana ambao wanaonekana wana kitu cha kufanya, lakini hawana msaada watashiriki kwa lengo la kupata msaada katika mfumo wa mtaji, mtandao na usimamizi wa ukuaji wa shughuli wanayofanya au kutaka kuifanya ili kuianzisha na kuikuza.

Mambo hayo yatatekelezwa katika mfumo wa shindano litakalogusa wajasiriamali ambao wana ari na nia ya dhati ya kuendeleza shughuli walizofikiria na kuzianzisha kwa lengo la kuinua uchumi wao binafsi na wa taifa.

Washindi watatu watakaotangazwa Aprili mwaka huu watapatiwa mtaji wa kuanzia au kuendeleza, pia watapatiwa maarifa ya kuendeleza shughuli zao na kuanzishwa mtandao wa kibiashara na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa MeTL Group na mwenyekiti wa Mo Dewji Foundation, Mohammed Dewji.

Wakati akipewa tuzo ya Forbes ya mwaka 2015, Mohammed Dewji aliitoa kwa heshima ya vijana akiwatakia kila la heri waking’aa, kuvunja nira ya woga, kukabili changamoto na kuendelea katika ujasiriamali kwa lengo la kufanya dunia yetu mahali bora pa kuishi.

No comments

Powered by Blogger.