Header Ads

Dkt. Mwakyembe awa mgeni rasmi Tamasha la Michezo la Wanawake

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, watendaji wa Wizara pamoja na washiriki wa Tamasha la Michezo la Wanawake lililoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa(BMT) 8 Aprili, 2017.


Na Mwandishi Wetu


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb) ameshiriki na kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Tamasha la Michezo la Wanawake lililoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).


Tamasha hilo limefanyika mapema leo 8 Aprili, 2017 katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Felix Lyaniva, pia washiriki mbalimbali toka kwenye Wizara, Taasisi za Serikali, binafsi pamoja na wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari.


Akihutubia hadhira iliyokuwepo uwanjani hapo, Dkt. Mwakyembe amewahamasisha wanawake kushiriki kikamilifu kwenye mazoezi mara kwa mara ili kulinda afya zao ikiwemo kuibua vipaji vya wasichana wadogo ambao ndiyo mbegu ya mafanikio katika sekta ya michezo.


“Serikali itaendelea kuipatia michezo kipaumbele kwa kuboresha Sera zote zinazogusa masuala ya michezo na elimu ya mazoezi ya viungo, kutenga bajeti ya kutosha kutoka katika ngazi zote kuanzia shuleni, vijijini, kata, Halmashauri/Wilaya, Mikoa, kutoa mafunzo mbalimbali pamoja na uhamasishaji wa ushiriki wa wananchi katika michezo”, alisema Dkt. Mwakyembe.


Aidha, ametoa rai kwa wananchi wote nchini kuachana na mila na tamaduni ambazo zinazuia wanawake kushiriki kwenye michezo.

No comments

Powered by Blogger.