TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameshiriki maziko ya Marehemu
Selemani Mrisho Kikwete ambaye ni Kaka wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete yaliyofanyika katika makaburi ya familia yaliyopo katika
kijiji cha Msoga, Wilaya ya BAgamoyo Mkoani Pwani.
Mzee Selemani
Mrisho Kikwete alifariki dunia tarehe 01 Machi, 2016 huko nchini India ambako
alipelekwa kwa ajili ya kupata matibabu ya saratani.
Pamoja na Rais
Magufuli viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo ni Makamu wa Rais
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Marais
wastaafu Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi na Mheshimiwa Benjamin William Mkapa,
Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa kwanza wa Rais na
Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa John Samwel Malecela, Viongozi wa dini na siasa
na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Akizungumza kabla
ya maziko, Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemshukuru
Rais Magufuli kwa kuungana na familia yake tangu wakati wa kuuguza, na hatimaye
maziko ya kaka yake Marehemu Mzee Selemani Mrisho Kikwete.
"Tumefarijika
sana kwa kuwa nasi wakati wote wa kuuguza na leo siku ya maziko, nakumbuka pale
wewe mwenyewe ulipohakikisha unasimamia matibabu ya kaka yangu alipokuwa nchini
India" Amesema Rais Mstaafu Kikwete.
Aidha, Rais
Kikwete amewashukuru viongozi wote na wananchi waliojitokeza katika mazishi ya
Marehemu Kaka yake.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
salaam
05 Machi,
2016
Post a Comment